Manara aahidi kuita Kariakoo “City Centre”

DAR ES SALAAM : MGOMBEA Udiwani wa Kata ya Kariakoo, Haji Manara, amewaahidi wafanyabiashara na wakazi wa kata hiyo kuwa endapo watampatia ridhaa ya kuwa Diwani, ataifanya Kariakoo kuwa “City Centre ya Saa 24”, kwa kuendeleza biashara na kutatua changamoto zilizopo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni zake leo Septemba 11, 2025, Manara alisema kuwa ana nia ya dhati kushirikiana na Halmashauri ya Jiji pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo ili kuunda mazingira bora ya biashara kwa wakazi wa Kariakoo.
“Kwangu mimi, biashara Kariakoo itaendelea kustawi. Kwa kushirikiana na Manispaa na Mbunge wetu, tutaendelea kuwapa fursa, kuwaheshimu na kuhakikisha wanafanya biashara kwa utulivu. Kariakoo hii tunayosema inalipa kodi sana itasinyaa,” alisema Haji Manara.
Manara pia ameahidi kuendeleza mradi wa wafanyabiashara kufanya biashara masaa 24, ikiwa ni pamoja na kufunga taa za sola na kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha usalama masaa yote. Amesisitiza kuwa wafanyabiashara watafanya biashara katika hali nzuri na salama. SOMA: Ni zamu ya Manara kuishika Dar kesho
Mbali na kuzingatia maslahi ya wafanyabiashara, Manara ameahidi pia kuheshimu haki za wakazi wa Kariakoo na kuhakikisha kuwa atawahudumia wote, bila kuepuka kundi lolote. Aidha, amewaomba wananchi kupuuza taarifa za mitandaoni zinazodai hana nia njema, akibainisha kuwa ni uzushi tu na lengo lake ni kuwatumikia wakazi wote wa Kariakoo.



