Manispaa Iringa yakosolewa mpango wa kukarabati ofisi zake

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amekosoa mpango wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa unaolenga kukarabati ofisi zake za sasa badala ya kujenga ofisi mpya akisema unaiondolea hadhi halmashauri hiyo.

Hatua ya manispaa hiyo kutaka kukarabati ofisi hizo imekuja baada ya taarifa iliyotolewa na Afisa Mipango na Uratibu wa manispaa hiyo Elias Mvula kuonesha maombi yao serikalini ya kupata fedha kwa ajili ya kujenga ofisi zake mpya katika eneo la Kihesa Kilolo kutozaa matunda.

Akitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha Baraza la Ushauri (RCC) la mkoa wa Iringa leo, Mvula alisema baada ya maombi yao ya kupata fedha serikalini kuonekana yanaweza kuchelewa walikuja na mpango mbadala wa kuboresha miundombinu ya ofisi zao za sasa ambazo kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa hazina hadhi inayofanana au kuzidi zile za halmashauri zingine za mkoa wa Iringa.

Afisa Mipango na Uratibu huyo alisema katika kuboresha miundombinu hiyo tayari wamepata mdau (hakumtaja jina) ambaye ameahidi kuchangia ukarabati huo wa ofisi hizo zenye ghorofa moja.

“Kuboresha jengo sikubaliani kabisa, kama mnataka vunjeni majengo yenu hayo na jengeni jengo lenye hadhi. Ninyi ndio sura ya mkoa wa Iringa kwasababu mpo makao makuu ya mkoa huu,” Dendego alisema.

Alisema kwa mazingira ya manispaa hiyo sio jambo la kujivunia “hata kidogo” kuwa na jengo la ghorofa moja moja kwa kuwa haikidhi mahitaji ya watumiaji au ina mapungufu kama vile nafasi ndogo, miundombinu duni, au huduma za msingi zisizotosheleza.

“Manispaa ya Iringa msituangushe, embu fikirieni kuwa na jengo kubwa ikiwezekana hata la ghorofa tano.

Mpo Prime Area, hili ni eneo lenye thamani kubwa au umaarufu zaidi katika mji wenu, fikirieni kufanya kitu kikubwa na kizuri zaidi,” alisema.

Akizungumzia mchango wa mdau huyo ambaye hakutajwa katika maboresho ya ofisi za manispaa hiyo, Mkuu wa Mkoa aliiagiza halmashauri hiyo kupokea mchango huo na kuuhifadhi wakati fedha na wadau wengine wakitafutwa ili kuwezesha mpango huo uwe bora zaidi.

Aidha aliiagiza halmashauri hiyo kupeleka ofisini kwake michoro ya maboresho wanayotaka kufanya ili iweze kufanyiwa kazi itakayokuwa na tija zaidi.

Mmoja wa wadau wa kikao hicho ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema halmashauri hiyo haina sababu ya kupoteza rasilimali fedha kwa kutekeleza mpango ambao mahitaji yake yanaweza kuwa ni ya muda mfupi.

Mdau huyo alisema; “mipango mibovu au kutokuwa na mahitaji ya sasa ya soko inaweza kusababisha maboresho kuwa na faida ndogo au kutokuwa na faida kabisa na hivyo kuathiri ufanisi wa halmashauri hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button