Manispaa Mtwara Mikindani kuchele

MTWARA; HALMASHAURI ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara kwa kutumia mapato yake ya ndani imefanikiwa kununua basi aina ya Tata kwa gharama ya Sh milioni 178.

Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa hafla fupi ya kupokelewa basi hilo leo Januari 19,2026 kwenye manispaa hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Mwalimu Hassan Nyange, amesema basi hilo litakuwa msaada mkubwa kwa manispaa kwani litapunguza matumizi hasa ya mafuta, ambapo baadhi ya safari badala ya kutumia magari mengine wanaweza kupanda basi moja.

‘’Pia tulikuwa tunakodi mabasi, hivyo sasa hatutakodi tena mabas, lakini pia shughuli mbalimbali kama vile kwenda kwenye nanenane na mengine tutakuwa tunatumia basi la halmashauri, ’’amesema Nyange.

Manispaa hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kupitia vyanzo vya mapato ya ndani ilipanga kukusanya zaidi ya Sh bilioni 7 na hadi kufikia Januari 18, 2026 halmashauri imekusanya zaidi ya Sh bilioni 5.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya ameipongeza manispaa kwa hatua hiyo ya kuwa basi zuri, hivyo wanapaswa kulitunza na kulitumia vizuri huku akitoa wito kwa wakurugenzi wengine kwenye wilaya hiyo kwamba hiyo iwe changamoto kwao.

Pia amefurahishwa na taarifa hiyo ya ukusanyaji wa mapato hayo kwenye mwaka huo wa fedha 2025/26 kupitia vyanzo vya ndani vya manispaa, kwani upo uwezekano kabla ya kuisha kwa mwaka huo wa fedha watavuka lengo kutokana na kasi iliyopo.

Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mipawa Elisha amesema lengo la kununua basi hilo ni kupunguza gharama za uendeshaji, kwani katika mikutano mingi walikuwa wakienda na magari mengi lakini sasa wataenda na gari moja, pia wananchi wanaona matokeo ya ushuru wanaoutoa kupitia shughuli zao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button