Maofisa utumishi ‘wenye uungu mtu’waonywa

SERIKALI: imewataka maofisa utumishi na wanasheria wa halmashauri kote nchini kuacha tabia ya kufanya kazi kwa misingi ya hisia, ukali na kiburi, na badala yake kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma, ili kulinda haki na kuongeza ufanisi wa utendaji.
Hayo yameelezwa kwenye Kikao Kazi cha Kutathmini Changamoto za Utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, Kanuni za mwaka 2022 na Usimamizi wa Maadili na Malalamiko, kinachofanyika mkoani Iringa kikihusisha maafisa utumishi na wanasheria kutoka mikoa ya Manyara, Dodoma, Singida, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa na Ruvuma.
Kikao hicho kinatekelezwa kwa mfumo wa kanda ili kuhakikisha halmashauri zote zinashiriki, tofauti na miaka ya nyuma ambapo halmashauri chache zilichaguliwa kwa kila mkoa.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Regina Ndege Qwaray, amewataka maafisa utumishi kuacha tabia ya kujiona “miungu watu” wakati wa kushughulikia changamoto za watumishi.
“Utumishi wa umma unaongozwa kwa sheria, miiko, miongozo na kanuni. Baada ya kikao hiki tunataka kuona mabadiliko. Wapo wanaokiuka sheria kwa kutokujua, lakini jukumu lenu ni kusimamia na kutafsiri sheria vizuri.”
Amesema rasilimali watu inapaswa kusimamiwa kwa weledi, kwani ikiharibika, utendaji na uchumi wa taifa hushuka.
“Ili taifa liwe na amani, ni lazima tufanye kazi vizuri. Wakiona wanatendewa haki, hata wale tunaowaongoza watafanya vizuri. Tujitafakari kama watumishi wetu wanaridhika.”
Akigusia tabia ya baadhi ya maafisa utumishi kuwa wakali na kutumia lugha mbovu, Qwaray alisema:
“Ni kweli mnasimamia sheria, lakini achaneni na ukali. Fungulieni milango, tumieni lugha nzuri. Acheni kujitapa nyinyi ni akina nani. Wasikilizeni watumishi wenu.”

Amesema mara nyingi mtumishi anapokuwa amegombana na mkuu wake wa idara, huenda kwa afisa utumishi kwa msaada, lakini anapokelewa kwa ukali zaidi na hatimaye anakosa mahali pa kukimbilia.
“Mnapaswa kuwapokea, si kuwaumiza zaidi. Waelekezeni kwa utaratibu,” alisema.Katika kauli yake, Qwaray aliwakosoa pia wanasheria wa halmashauri wanaosimamia mashauri ya nidhamu.
“Wanasheria wamekuwa wakisababisha haki kuuzwa kwa sababu hawajalipwa vizuri. Hii si sababu. Tutafsiri sheria vizuri na tutende haki. Sio kila mtu ana uelewa wa sheria tuwasaidie.”
Awali, Kaimu Katibu Mkuu Utumishi ambaye ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Felista Shuli alisema:
“Kikao kinalenga kuimarisha utendaji na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi, kufuatia ongezeko la malalamiko na kushuka kwa uwajibikaji katika baadhi ya halmashauri.

Amesema baadhi ya watumishi wamekuwa wakifanya kazi bila kufuata sheria na miongozo, jambo linalochangia mashauri ya kinidhamu kuongezeka na serikali kupata hasara.
“Kuna kasumba ya kutofuata sheria, miongozo na nyaraka mbalimbali kwa makusudi au kwa kutokuelewa. Kikao hiki kitawaelimisha namna ya kupunguza changamoto hizo. Malalamiko ni mengi, yanathibitisha watu hawawajibiki.”
Amesema si aibu kwa maafisa kuomba miongozo pale wanapokosa uelewa, kwani majibu yanapatikana wazi katika sheria, kanuni na nyaraka za serikali.



