Maombi ya Ngajilo kituo cha Afya Uyole yazaa matunda

IRINGA: Maombi ya Mgombea Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya CCM, Fadhili Ngajilo, kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Kituo cha Afya Uyole kata ya Kitwiru yameanza kuzaa matunda, baada ya Serikali kuidhinisha Sh milioni 50 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni mwendelezo wa ahadi aliyotoa wakati wa kampeni katika Kata ya Kitwiru, ambapo wananchi walilalamikia kituo hicho kushindwa kutoa huduma kwa muda mrefu.
Ngajilo aliwaahidi kwamba ndani ya siku 100 za ubunge wake, kituo hicho kingeanza kutoa huduma bora na sasa ahadi hiyo inaanza kutimia.
Wananchi wa Kitwiru na makada wa CCM wamepongeza hatua hiyo, wakisema ni ushahidi wa uongozi makini wa kijana huyo ambaye anatambulika kwa kasi na utekelezaji wa vitendo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Gangilonga, Ibrahim Ngwada, alimuelezea Ngajilo kama msomi mwenye maono, bidii na moyo wa kujituma.
“Ngajilo ni msomi mwenye shahada mbili. Ni kijana mwenye spidi ya maendeleo na moyo wa kujitolea. Huyu ndiye kiongozi tunayemhitaji Iringa,” alisema Ngwada.
Katibu wa CCM Iringa Mjini, Hassan Makoba, alisema Ngajilo ni mfano wa viongozi wa kizazi kipya wanaohitajika leo vijana wachapakazi, wasikivu na wanyenyekevu.
“Hana majungu, hana makuu. Ni mpenda watu, na yuko tayari kutatua changamoto za wananchi wake kwa vitendo,” alisema Makoba.
Kwa upande wake, mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa, Tumaini Msowoya aliwaasa wananchi kuendelea kuienzi amani ya nchi na kuepuka siasa za mgawanyiko.
“Tuchague chama kilicholeta maendeleo na amani. Tusiwe kama wenzetu wanaosikia milipuko ya mabomu kila siku. Tuitunze amani yetu, tuchague CCM,” alisema.
Mratibu wa Kampeni za CCM Iringa Mjini, Salvatory Ngerela, alisema kampeni za chama hicho zimejikita katika kueleza mafanikio halisi yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, hususan katika sekta za afya, elimu, kilimo na miundombinu.
“CCM hatuendeshi kampeni za maneno. Tunazungumza yale tuliyofanya na tunayopanga kufanya. Tunakuja kuomba ridhaa ya kuendeleza tulichoanza,” alisema Ngerela.
Kupitia taasisi yake, Ngajilo Foundation for Development and Democracy, mgombea huyo ameahidi kushirikiana na vyuo vikuu vilivyopo Iringa kuibua mawazo mapya ya maendeleo, kuwawezesha wanawake, vijana na wazee, pamoja na kuimarisha mazingira ya ujasiriamali.
“Tunataka Iringa iwe kitovu cha fursa. Tutashirikiana na taasisi za kifedha na vyuo vikuu kuhakikisha wananchi wanapata nguvu ya kiuchumi,” alisema Ngajilo.



