Mapya yaibuka kibano namba za 3D

DAR ES SALAAM: Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, limefafanua kwa nini wameanza oparesheni ya kung’oa namba za magari zenye mfumo wa 3D.

Akizungumza leo Februari 29, 2024 Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Ramadhani Ng’anzi, amesema vifaa vyao vinashindwa kutambua gari zenye namba za usajili za mfumo wa 3D ikiwa mbali, ndio maana wanazing’oa kwa ajili ya usalama na kuongeza kuwa kwa namba hizo mtu anaweza kufanya uhalifu na kuzitupa.

“Unapoweka 3D herufi zinakuwa kubwa, kunakuwa na kivuli, pia ‘material’ wanayotumia haikubaliki rangi nyeusi tu wanazozijua wao huko mitaani, gari ikiwa mbali huwezi kuijua mpaka wafike karibu, wakati mwingine magari yanapita kwa kasi unashindwa kuitambua hata kama imefanya makosa barabarani,”amesema Kamanda Ng’anzi.

Amesema kuweka 3D kwenye gari ni kukiuka sheria za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sheria ya Usalama Barabarani na ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), inayosema kuweka nyongeza bila kibali cha usalama barabarani ni kosa kisheria na hatua zitachukuliwa kwa wahusika ikiwemo kuendelea kuving’oa vibao hivyo.

“Mawakala wetu wamepewa plate namba ilivyopendekezwa na TBS tukiruhusu mtaani kila mtu atengeneze plate namba huko mtaani itakuwaje kiusalama?” Amehoji na kuongeza:

“Kwa mawakala wetu unapokwenda unasubmit kadi yako ya gari huko mtaani wanakotengeneza wanasubmit nini? Mtu anaweza kufanya uhalifu huko mtaani akachomoa vibao na kutupa utajua ni nani?

“Kuna vitu kama jamii inahitaji 3D mfumo ufuatwe ili tutoke kwenye 2D na kwenda kwenye 3D kisheria, ”amesema

Habari Zifananazo

Back to top button