Marekani yasifu ubora SGR

BALOZI wa Marekani nchini, Michael Battle ameisifia treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kwa huduma bora na huku akisema amesafiri mabara manne duniani ila anajivunia huduma bora ya usafiri wa treni hiyo kwa Tanzania.
Kauli hiyo ameitoa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X jana alipoweka ujumbe huo na picha yake aliyoipiga akiwa nje ya sehemu ya mabehewa ya treni hiyo.
Aliandika: “Treni kutoka Dar kwenda Dodoma. Nimepanda treni kwenye mabara manne na ninajivunia kusema kuwa Tanzania inatoa uzoefu bora wa kipekee wa treni. Treni iliondoka stesheni kwa wakati, safari ilikuwa ya starehe, ukarimu na umahiri wa watoa huduma bora ndani ya treni”.
Pongezi hizo ni fahari kwa Watanzania kwa kazi nzuri inayoendelea kufanywa na serikali kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo.
Lakini pia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2020 – 2025 inayosisitiza kuwaletea wananchi maisha bora na mazuri.
Usafiri wa treni ya SGR kwa abiria ulianza Juni 14, mwaka jana kwa safari za treni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Julai 25, mwaka jana ulifanyika uzinduzi wa safari hizo kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ulifanywa.
Rais Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi usafiri huo Agosti Mosi, mwaka jana kwa kupanda treni kutoka Stesheni ya Magufuli, Dar es Salaam hadi Stesheni ya Samia Dodoma akipita katika vituo mbalimbali ikiwamo Stesheni ya Jakaya Kikwete, Morogoro.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, safari za SGR zimeiingizia serikali zaidi ya Sh bilioni 3.1 tangu zilipoanza.



