Masauni ataka elimu zaidi usimamizi mazingira

DODOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuweka nguvu zaidi katika utoaji wa huduma na elimu kwa umma kuhusu sheria ya usimamizi wa mazingira, ili kuhakikisha utunzaji wa mazingira unakuwa endelevu nchini.

Mhandisi Masauni ametoa agizo hilo leo wakati wa kikao kazi na Menejimenti ya NEMC kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Baraza, jijini Dodoma.

Amesema kuwa baraza lina jukumu kubwa la kuhakikisha Mazingira yanatunzwa na ili suala hilo lifanikiwe ni lazima kila mmoja  kutimiza majukumu yake katika uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira.

 

Aidha, Waziri Masauni amewaasa Watanzania kuacha kuchukulia poa suala la utunzaji wa mazingira na badala yake kuwajibika katika kuyatunza ili yaendelee kuwa maeneo salama ya kuishi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Sware Semesi, alimshukuru Waziri kwa kuonesha ushirikiano kwa menejimenti ya baraza na kwa kusikiliza maoni mbalimbali yaliyotolewa kwa lengo la kuboresha utendaji wa baraza na ustawi wa taifa kwa ujumla.

Kikao hicho kimekuwa sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha taasisi zinazohusika na mazingira zinatimiza majukumu yake kikamilifu kwa manufaa ya taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button