Masharti ufugaji, faida uhifadhi fisi

“SERIKALI inaruhusu kisheria ufugaji wa wanyamapori wakiwamo fi si, lakini kanuni na sheria haziruhusu kufuga mnyamapori mmoja mmoja, badala yake zinaruhusu kufuga wanyamapori kwa ngazi ya bustani au shamba la wanyamapori.”
Anasema Ofisa Habari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Beatus Maganja anapozungumza na gazeti la HabariLEO kuhusu kuuawa kwa fisi 17 na kukamatwa kwa mtu mmoja akidaiwa kufuga fisi nyumbani kwake mkoani Simiyu.
Hayo yanajiri katika operesheni ya hivi karibuni iliyoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kutekelezwa na Tawa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, likiwamo Jeshi la Polisi ambalo kupitia operesheni yake kupambana na uhalifu na wahalifu, Januari 24, 2025 lilimkamata Emmanuel Maduhu (31) kwa tuhuma za kuwa na fisi nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe mtuhumiwa huyo ambaye ni mganga wa jadi alikutwa na fisi akiwa anamfuga nyumbani kwake katika Kijiji cha Kilulu, Kata ya Bunhmala wilayani Bariadi.
Swebe anasema baada ya mahojiano, mganga huyo alisema amekuwa akimtumia fisi huyo kwa shughuli zake, ikiwa ni pamoja na kumtumia kama chombo cha usafiri kwenda maeneo mbalimbali kwa ajili ya shughuli zake za uganga. Kwamba, ili kufika Tanga hutumia muda wa saa mbili na saa moja kutoka Simiyu hadi mkoani Kagera.
Vyanzo mbalimbali vilivyoshuhudia tukio hilo la fisi mkoani Simiyu vinabainisha kuwa alikuwa na shanga pamoja na namba kama zinazowekwa kwenye vyombo vya moto kama magari na pikipiki Ingawa suala hili halina uthibitisho wa kisayansi kuhusu ukweli wake, habari kutoka vyanzo mbalimbali zinasema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia fisi kwa mambo ya kishirikina kama chombo cha usafiri.
Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo na zawadi kwa askari polisi waliofanya kazi vizuri katika utendaji kazi wao tuzo zilizotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IJP), Camillius Wambura, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi alisema operesheni ililenga kutafuta fisi ambao wamekuwa wakisumbua wananchi, ikiwemo na kung’ata watoto.
Kihongosi anasema katika operesheni hiyo baadhi ya watu walikamatwa kutokana na kubainika wakifuga wanyamapori hao nyumbani.
Akisisitiza kuwa fisi si chombo cha usafiri, bali mnyama anayetakiwa kuishi porini au hifadhini, mkuu wa mkoa anasema, “Nitoe onyo kali kwa wale wanaomiliki fisi kwa matumizi mbalimbali, tutachukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika maana ni kinyume cha sheria kuishi au kufuga fisi…”
Anaongeza: “Hili jambo halipendezi hata kidogo, linauchaufua mkoa wetu, Mkoa wa Simiyu unayo mambo mengi mazuri, mambo ya kumiliki fisi hayakubaliki hata kidogo, kwanza ni kosa la jinai.” Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mpepele anasema operesheni hiyo ni sehemu ya mkakati endelevu wa serikali kupambana na wanyama wakali na waharibifu.
Anasema ingawa jamii inapenda wanyama na uhifadhi, maisha ya watu ni kipaumbele cha kwanza. “Uhifadhi ukiimarika, utazidi kuvutia utalii kama tunavyoshuhudia ongezeko la watalii kutokana na juhudi za Rais samia Suluhu Hassan ambaye ni Mhifadhi Namba Moja… lakini lazima uhifadhi huu uende sambamba na usalama wa watu,” anasema Mapepele.
Akijikita katika kanuni zinazoruhusu ufugaji wa fisi kama wanyamapori wengine wowote kwa mujibu wa sheria, Ofisa Habari huyo wa Tawa anasema eneo la kufugia wanyamapori lazima liwe limefanyiwa tathmini ya kina kuhusu athari za kimazingira kubaini kama linafaa kwa kazi hiyo bila kusababisha athari mbaya katika mazingira, kwa watu
na kwa wanyama husika.
Anasema, “Eneo hilo halipaswi kuwa karibu na makazi ya watu… na maombi lazima yapelekwe kwa Kamishna wa Uhifadhi wa Tawa kuhusu mradi au biashara hiyo kupata na kupata usajili BRELA (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni)…”
Kwa mujibu wa Tawa, bustani ya wanyama ni mahali ambapo wanyamapori wa aina mbalimbali hutunzwa kwa ajili ya kutazamwa na watu.
Tawa katika tovuti yake inabainisha utaratibu wa kuanzisha maeneo ya ufugaji wanyamapori ikisisitiza kuwa, husimamiwa na Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, Kanuni ya Usimamizi wa Maeneo ya Ufugaji Wanyamapori za Mwaka 2020 na Kanuni za Leseni ya Biashara ya Nyara za Mwaka 2010.
Kwa mujibu wa Maganja, ili kupata leseni ya kuanzisha eneo la ufugaji, mwombaji anatakiwa kuwasilisha maombi kwa Kamishna wa Uhifadhi kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa katika Kanuni 4 – 7 ya Kanuni za Usimamizi wa Maeneo ya Ufugaji Wanyamapori za Mwaka 2020.
Hizi ni pamoja na mwombaji kuwa ni Mtanzania na kama ana ubia na mtu ambaye si Mtanzania, lazima asilimia 51 ya hisa ziwe za Mtanzania huyo.
Mengine ya lazima kutimiza ni pamoja na mwombaji kuwasilisha Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), kuwasilisha uthibitisho wa umiliki wa ardhi, kuwasilisha uthibitisho wa kwamba mradi unaendana na matumizi ya ardhi ya eneo hilo pamoja na kuwasilisha mpango wa biashara.
Kuhusu aina za maeneo ya ufugaji, Tawa inasema ni bustani ya wanyamapori, shamba la wanyamapori/ Eneo la uzalishaji wanyamapori na ranchi ya wanyamapori. Kwa mujibu wa Maganja, ufugaji katika bustani za wanyamapori ni kwa ajili ya elimu, utafiti na burudani.
Anasema, “Bustani ya wanyamapori huanzishwa katika eneo dogo hadi kubwa kulingana na aina na idadi ya
wanyamapori wanaopendekezwa kufugwa.”
Inaongeza: “Ufugaji katika shamba la wanyamapori hufanywa katika eneo lisilopungua hekta 500 na lisilozidi hekta 2,000 kwa ajili ya matumizi ya uvunaji na yasiyo ya uvunaji”.
Tawa katika moja ya machapisho yake mtandaoni inasema, “Eneo la uzalishaji huanzishwa katika eneo kubwa au dogo kulingana na aina na idadi ya wanyamapori wanaopendekezwa kwa ajili ya matumizi ya uvunaji na yasiyo ya uvunaji.”
Kwa mujibu wa Maganja, kukutwa na mnyamapori ama aliye hai au aliyekufa au hata kiungo au sehemu yoyote ya mwili; iwe kucha, meno, ngozi, nyama au hata mkia ni kosa kisheria kwa kuwa ni kumiliki nyara za serikali kinyume cha sheria…”
Anaongeza kuwa, ni kuhujumu uchumi kwa kuwa lazima kuna mnyamapori ameuawa. Mwenyekiti wa Waganga
wa Tiba Asili na Tiba Mbadala katika Mkoa wa Simiyu, Mayunga Kidoyai anasema, “Wapo wanyamapori wanaofugwa kwa kuonekana kwa macho kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa nyara hai na nyara mfu…”
Anaongeza: “Wapo baadhi ya watu ambao hufuga wanyamapori hai kwa mambo mabaya, yakiwamo ya kishirikina na ndio hao wengine kama fisi wanakamtwa wakiwa na ‘plate number’ (namba za usajili) ili kujulikana kuwa huyu
ni mali ya mtu na kwamba, kuna wengine”.
Anapongeza juhudi zilizofanywa na serikali ya mkoa, wilaya, viongozi na wananchi wengine kuelimisha umma dhidi ya imani potofu za ushirikina. Imani hizi ni pamoja na matumizi mabaya ya nyara za serikali kama wanyapori, hali inayochochea uelewa kwa watu kiasi cha baadhi ya wanaowatumia kinyume na sheria kuamua kuachana na
wanyamapori hao.
“Hao, ndio mnaona sasa wazagaa hadi mijini maana… Kufanya ushirikina dhidi ya mtu hata kama ni kiongozi ili
asifanikiwe katika uongozi wake ni uhujumu kwa taifa. Mtu anaona hakuna haja kukaa nayo (fisi) kama amepata elimu sahihi na sasa ameelewa hakuna sababu ya kukaa nayo,” anasema.
Kidoyai anasema ipo haja jamii ikaungana kuelimisha umma zaidi ili kuachana na imani potofu ambazo zimekuwa zikisababisha madhara kwa jamii, yakiwamo mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
Mkazi wa Dar es Salaam aliyekataa kutajwa, anasema elimu inayotolewa kwa umma ihusishe pia, kuhamasisha wanaomiliki wanyama hao kujua namna ya kuwaachia ili wasiende kufanya madhara kwa watu.
“Wanaomiliki au kufuga wanyamapori kama fisi kinyume cha sheria, wapewe muda maalumu wa kusalimisha kwa hiari katika mamlaka zinazohusika na wanyamapori na wasichukuliwe hatua zozote zaidi ya msamaha…” anasema.
Faida kubwa ya fisi
Vyanzo mbalimbali vinamtaja fisi kuwa ndiye ‘bwana afya’ wa porini kwa kuwa hushughulika zaidi na mizoga na pia, mizoga ndiyo chakula chake kikubwa. Chanzo kimoja kinasema mtandaoni: “Fisi akikuta mizoga, anafanya kusafisha
anapita nayo (anakula), fisi ndiye msafishaji wa porini ingawa hii haina maana kuwa hawindi, hapana lakini ni kwa nadra sana.”
Makala haya yameandaliwa na Derick Milton na
Joseph Sabinus



