Mashine zaidi ya 100 kupunguza gharama usafishaji figo

ILI kupunguza gharama za matibabu ya kusafisha figo nchini, Serikali imesambaza mashine zaidi ya 100 pamoja na vitendanishi vyake katika hospitali za rufaa za mikoa mbalimbali nchini.

Taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 8, 2025 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, wakati akijibu swali kuhusu mipango ya serikali kupunguza gharama za huduma za kusafisha figo nchini.

Dk. Mollel amesema mbali na usambazaji wa mashine hizo, serikali pia imeongeza vituo vya kutoa huduma ya ‘dialysis’ katika hospitali 15 za rufaa za mikoa na hospitali zote za kanda, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi wengi zaidi.

Katika kuhakikisha ushindani wa bei na upatikanaji wa vifaa tiba, Dk. Mollel amesema serikali ina mpango wa kuongeza wadau na taasisi zinazohusika na uingizaji wa vitendanishi, dawa na vifaa tiba vinavyotumika kwenye huduma hiyo, badala ya kuruhusu kampuni au taasisi moja kutawala soko.

Aidha, Dk. Mollel amewahimiza wananchi kujiunga na mfumo wa bima ya afya mara tu utakapozinduliwa rasmi, akibainisha kuwa huo ndio utaratibu bora na wa uhakika utakaosaidia wananchi kujikinga dhidi ya gharama kubwa za matibabu.

Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha huduma za afya na kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa gharama nafuu kwa Watanzania wote.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button