Mashirika ya vijana yafundwa kukabili mabadiliko tabianchi

WAWAKILISHI kutoka mashirika 10 yanayoongozwa na vijana, ambayo ni watekelezaji wa Mradi wa Vijana A@rtwork, wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo umuhimu wa kutumia Sanaa kama nyenzo ya kuleta mabadiliko na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza katika mafunzo hayo ya siku mbili Dar es Salaam leo Meneja wa mradi huo, Mandolin Kahindi amesema lengo kuu ni kuyawezesha mashirika ya vijana kuboresha utekelezaji wa miradi yao kwa kuzingatia usimamizi wa miradi na fedha, ufuatiliaji na tathmini, pamoja na mawasiliano na uonekano wa miradi kwa umma.

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa mradi kuhakikisha washirika wanatimiza kwa ufanisi ahadi zao za kuwahusisha vijana, wanawake na jamii katika kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia pamoja na ajira kwa vijana.

“Mashirika haya yanatumia nyenzo za Sanaa kama filamu, maigizo, redio za jamii, majadiliano ya kijamii na mikutano mbalimbali ili kuchochea mazungumzo ya jamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi, nafasi ya Sanaa katika maendeleo na fursa za ajira kwa vijana,” amesema Kahindi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ladies Joint Forum, Fransica Mboya ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo, amesema mafunzo hayo ni fursa muhimu itakayowawezesha kutekeleza miradi yao kwa weledi zaidi.

Amesema mradi wao unatekelezwa wilayani Misungwi mkoani Mwanza, ukilenga kuimarisha usawa wa kijinsia kwa kutumia filamu, na kwamba mafunzo hayo yatawasaidia kuwafikia wanawake na wasichana kwa ufanisi zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Asedeva, Isack Abeneko amesema wao ni wanufaika wa mradi huo katika eneo la Kinondoni, ambapo wataimarisha matumizi ya Sanaa kama chombo cha kuibua na kujadili changamoto za kijamii.

“Tutatumia maigizo, ngoma na muziki kubuni maudhui yanayotokana na jamii yenyewe ili kuwahamasisha wananchi kuzungumza na kushiriki katika kutatua changamoto zinazowakabili,” amesema Abeneko.

Mradi huo unatekelezwa na Kituo cha Utamaduni cha Ujerumani hapa nchini Goethe-Institute kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Sanaa Afrika Mashariki (CDEA), kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button