Mashirika yaagizwa umakini kuepuka hasara

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu ameagiza vitengo vya sheria katika mashirika ya umma kuiepusha serikali hasara katika mikataba ya kibiashara.
Mchechu ametoa agizo hilo katika kikaokazi cha wadau kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kinachofanywa katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
SOMA: Mashirika yaliyofanya vizuri yakabidhiwa tuzo
Amesema ofisi yake inasimamia mashirika 308, yakiwemo 252 ambayo serikali ina umiliki wa moja kwa moja.
“Hapa ni lazima kuwa makini kwa sababu mikataba ni eneo nyeti, linaweza kupoteza fedha nyingi au kuokoa. Lazima Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ahusishwe ili kuepuka hasara au kuharibu taswira ya taifa,” amesema Mchechu.
Ameongeza: “Sasa niwatake wakuu wa vitengo au mameneja wa sheria katika taasisi zote zilizo chini ya ofisi yangu wahakikishe wanatambua wao ni sehemu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wana wajibu wa kwenda sambamba na miongozo ya ofisi hiyo ili kuleta tija kwa taifa”.
Mchechu ameagiza wahakikishe mambo hatarishi kisheria au mambo ya kulinda maslahi ya taifa na umma yanawasilishwa haraka na kwa usiri kwenye ofisi ya mwanasheria mkuu.
Mchechu amesema uwekezaji umeongezeka kwa asilimia saba kufikia Sh trilioni 92.29 Juni 30, 2025 kutoka Sh trilioni 86.3 katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Amesema uwekezaji huo unahusisha mashirika ya umma 255 na kampuni 45 ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache na taasisi za kigeni 10 ambazo kwa pamoja zinatengeneza uti wa mgongo wa mapato yasiyo ya kodi ya Tanzania.
Aidha, amesema katika kipindi cha miaka mitano, uwekezaji wa ndani umeongezeka kutoka Sh trilioni 67.01 mwaka 2020/21 hadi kufika Sh trilioni 90.61 mwaka 2024/25, hali inayodhihirisha utendaji bora na usimamizi ulioboreshwa katika mashirika ya umma.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno amesema taasisi zote za serikali zimeunganishwa na Mfumo wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Umma (NeST).
Maneno amesema kabla taasisi, shirika au wakala wa umma hajaingia mkataba na mtoa huduma au mzabuni,
lazima Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali aupitie na kujiridhisha kama una tija au la.