Mashirika yaliyofanya vizuri yakabidhiwa tuzo

ARUSHA: MASHIRIKA ya Umma yaliyofanya vizuri katika mwaka wa fedha 2023/24 yamekabidhiwa tuzo maalum na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika hafla rasmi iliyofanyika kwenye Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma.

Tuzo hizo zilikabithiwa jana Jijini Arusha katika kikao kilichofunguliwa na Makamu wa Rais Dk, Philip Mpango ambazo zilizingatia vigezo vya kiuendeshaji kama vile ukuaji wa mapato ya ndani, udhibiti wa matumizi, kuimarisha faida (Net margin), kuboresha ukwasi (Current ratio) na rejesho la uwekezaji (ROE).

Vigezo vingine ni kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali, ufanisi katika matumizi, utekelezaji wa hoja za kikaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uchapishaji wa taarifa za fedha, na maboresho ya utoaji huduma kwa jamii.

Taasisi zilizotunukiwa zilitangazwa chini ya makundi manne mahsusi kulingana na aina na majukumu yao ambapo kundi la mashirika yanayofanya biashara, tuzo zilitolewa kwa mashirika yaliyoboresha mapato, faida, ukwasi na rejesho kwa mtaji wa serikali.

Washindi wa kundi hili walikuwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bohari ya Dawa (MSD) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),Mashirika mengine yaliyofanya vizuri katika kundi hili ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Kwa mashirika yasiyofanya biashara, vigezo vilihusisha udhibiti wa matumizi, kuimarisha mapato ya ndani, kudhibiti matumizi na kupunguza utegemezi kwa ruzuku ya Serikali.

Washindi walikuwa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB Tobbaco) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Taasisi nyingine ni Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Bima (TIRA.

Katika kundi la mashirika yanayofanya na yasiyofanya biashara kwa kigezo cha utawala bora, tuzo zilitolewa kwa mashirika yaliyotekeleza kwa kiwango cha juu hoja za ukaguzi, kupata maoni chanya ya ukaguzi, kuchapisha taarifa za fedha na kuwa na tathmini nzuri ya bodi.

Ambapo Washindi katika kundi hili walikuwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Taasisi nyingine zilizofanya vizuri ni pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi kwa Umma (PPRA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA)

Kwa upande wa utoaji wa huduma bora kwa jamii, tuzo zilitolewa kwa taasisi zilizoboresha mifumo ya kidijitali, kuongeza kiwango cha kuridhika kwa wateja na kufanikisha ongezeko la walengwa wa huduma.

Taasisi zilizoshinda tuzo hii ni Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani (WRRB) na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button