Matukio mwaka 2024; Treni ya kisasa SGR yaanza kutoa huduma

MWAKA 2024 Tanzania iliandika historia nyingine ya kuanza usafiri wa Treni ya Kisasa (SGR).
Historia hiyo ilianza Juni 14 kwa safari za treni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na baadaye kutoka Dar es Salam hadi Dodoma, Julai 25.
Treni za SGR zipo za aina mbili, ile ya kawaida na ile ya mchongoko (ya haraka) na kwa mujibu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) mpaka sasa zaidi ya abiria milioni moja wametumia usafiri huo kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na Dodoma.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa safari za treni hiyo ya kisasa zimeiingizia serikali zaidi ya Sh bilioni 3.1 tangu zilipoanza.
Seti ya kwanza ya treni ya kisasa ya umeme (EMU), vichwa vitano vya umeme na mabehewa matatu ya abiria vilianza kuwasili kwenye bandari ya Dar es Salaam mapema Machi mwaka huu.
Seti moja ya Emu ina uwezo wa kubeba abiria 589 na kutembea kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa.
SGR ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ambayo serikali imeamua kuifanya na itakapokamilika inatarajiwa kuwa mkombozi wa usafiri wa abiria na mizigo.

Ujenzi wa SGR ulianza mwaka 2017 kwa kipande cha kilometa 300 kinachoanzia Dar es Salaam kwenda Morogoro ambacho kilizinduliwa na Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli Aprili 12, mwaka huo.
Baadaye ujenzi wa kipande cha pili cha kilometa 442 cha kutoka Morogoro hadi Makutupora ulizinduliwa Machi 14, 2018.
Kukamilisha mradi huo ni kama kutimiza ndoto kwani mpango wa kujenga reli hiyo ulianza tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa na kukamilika Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Wazo la kujengwa reli hiyo lilianzia kwa Mkapa baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, wakilenga kujenga reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Kigali Rwanda, miaka 29 iliyopita.
Rais Samia alipoingia madarakani Machi 2021 alikuta mradi ulishaanza kujengwa kwa urefu wa kilometa 722 na hadi sasa umefikia kilometa 1,522 kwa viwango tofautitofauti.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa safari za Dar es Salaam kwenda Dodoma, Agosti Mosi mwaka huu, Rais Samia alisema anajisikia faraja kuona miradi aliyoianza kuitekeleza tangu awamu ya tano, ikiwamo Daraja la Tanzanite, Bwawa la Umeme la Nyerere (JNHPP) na SGR inakamilika na kuwahudumia wananchi.
“Licha ya mradi huu (SGR) kuwa na ugumu katika utekelezaji wake lakini imefikia hatua nzuri na sasa inahudumia wananchi kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma,” alisema.
Rais Samia alisema anachukulia mradi huo kama sehemu ya kutoa huduma kwa jamii na kuiletea maendeleo makubwa, hivyo hatarajii mradi huo uanze kutoa faida haraka.
Alisema ujenzi wa reli hiyo unaendelea hadi Kigoma, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupanua biashara za kimataifa.
Rais alisema alisukumwa kutekeleza mradi huo uliogharimu takribani Sh trilioni 10 na kuiunganisha nchi na mataifa Jirani, ikiwamo DRC ili kufungua fursa za biashara.

Alisema licha ya treni hiyo kubeba abiria pia itatumika kusafirisha mizigo ya kibiashara kama mafuta tofauti na awali yalipokuwa yakisafirishwa na malori.
Rais Samia aliwataka Watanzania kutumia fursa ya treni ya kisasa iliyoanza kwa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo zinakazowaingizia mapato kupitia masoko ya ndani na nje.
Alisema Watanzania wanapaswa kuongeza nguvu ya uwekezaji kwenye kilimo na shughuli zingine ili kukuza biashara kwa kutumia usafiri wa treni.
Aidha, Rais Samia alizipa majina stesheni za SGR na sasa kuna John Magufuli (Dar es Salaam), Jakaya Kikwete (Morogoro), Samia (Dodoma), Tabora itaitwa Ali Hassan Mwinyi na Shinyanga itaitwa, Abeid Amani Karume, Mwanza itaitwa Julius Nyerere na Kigoma Benjamin Mkapa.

Kwa mujibu wa Kadogosa treni hiyo pia inatumiwa na wasafiri wa mikoa ya mbali kama Mwanza ili kupunguza muda wa safari ambao wangetumia kama wangepanda mabasi ya kawaida.
“Wanapofika Dodoma wanapanda mabasi ya kwenda Mwanza, Iringa, Arusha, Kagera na mikoa mingine. Kwa hiyo mtu akitoka saa 12:00 asubuhi, anafika Dodoma na kuchukua basi saa 4:00 na anafika Mwanza saa 11:00 au 12:00 jioni wakati awali walikuwa wanafika saa 8:00 usiku,” alisema.



