Matumizi kuni, mkaa taasisi za umma mwisho leo -Majaliwa

LINDI: WAZIRI Mkuu wa Nchi, Kassim Majaliwa Majaliwa amezikumbusha taasisi na mashirika yote ya Serikali yaliyopo kote nchini Tanzania ambayo yanahudumia watu zaidi ya 100, kutekeleza bila shuruti agizo lake la kuitangaza Desemba 31, 2024 kuwa siku ya mwisho kwa matumizi ya mkaa na kuni kwenye shughuli za mapishi.
Majaliwa ametoa kauli hiyo mapema leo wakati akihutubia wananchi kwenye Tamasha la Azimio la Kizimkazi 2024, linalofanyika kwa mara ya pili Ruangwa mkoani Lindi ikiwa ni mara baada ya kuzinduliwa kwake mapema mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan, Kizimkazi Visiwani Zanzibar.
Aidha, Majaliwa amezitaja taasisi zinazohusika na agizo hilo kuwa ni pamoja na taasisi zote zenye kuhudumia watu zaidi ya mia moja ikiwemo majeshi mbalimbali, shule za bweni za binafsi na za serikali, magereza pamoja na wazabuni wanaopika vyakula vya zaidi ya watu 100 ambapo lengo ni kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ili kuondokana na athari za kiafya na uharibifu wa misitu unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Katika kutekeleza Lengo hilo la mwaka 2034, Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na halmashauri zote nchini Tanzania kuhakikisha kuwa ajenda ya matumizi ya nishati safi inakuwepo kwenye mikutano na shughuli zao mbalimbali kwa kutoa hamasa kwa wananchi juu ya faida ya matumizi ya nishati safi na athari za matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
Pia Majaliwa ametaja uwepo wa magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya macho, Pumu, mapafu, maumivu ya kifua na magonjwa ya moyo kama miongoni mwa athari zinazowakumba kinamama na wasichana wengi kutokana na kutumia kuni na mkaa kwenye kupika vyakula.
Uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kampeni ya kimataifa katika juhudi za kutunza mazingira na afya za watu ambapo nchini Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan ametajwa mara kadhaa kuwa linara barani Afrika na duniani kote katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi suala ambalo limepelekea Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa hamasa ya matumizi ya nishati safi, mkutano unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari mwaka 2025.