MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema ofisi yake inakuja na Meza ya Msemaji Mkuu wa Serikali.
Amesema hatua hiyo itaruhusu wanahabari na wananchi kupata taarifa kutoka kwa viongozi wakuu wa wizara na taasisi kuhusu maendeleo yanayofanywa na serikali.
Msigwa alisema hayo juzi wakati akifunga mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari uliohusu mafanikio ya ukuzaji wa uwekezaji na maboresho ya mazingira ya biashara 2024 na mwelekeo wa 2025, ulioandaliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
“Mhe Rais aliturudishia Wizara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali nikajiuliza nitoke vipi! kwa hiyo nakuja na Meza ya Msemaji Mkuu wa Serikali ambayo tutakuwa tunawaita waheshimiwa mawaziri, watakaa watazungumza na waandishi wa habari,” alieleza.
Aliongeza, “Na nataka niende mbali zaidi nataka mpaka wananchi waulize maswali moja kwa moja kwa waheshimiwa mawaziri, tutatengeneza utaratibu mzuri kwa msaada wa teknolojia ili tutakapoanza meza hiyo, tuvifikie vyombo vyote vya habari kwa watakaoweza kuja na wasioweza kuja, yaani mtu afikiwe na taarifa popote alipo”.
Alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, inafanya mambo makubwa ya maendeleo, hivyo viongozi wanatakiwa kuyasema kwa wananchi na kupitia meza hiyo watapata fursa ya kuyajua mambo mengi.
Msigwa alisema kwa kuanzia, mwezi huu itaanza mikutano ya taasisi katika kutimiza lengo la wananchi kupata taarifa.
“Taarifa za meza hii zitafika mpaka kwenye vyumba vya habari, kwenye televisheni na kwenye simu yako ya mkononi, nawasubiri wanasayansi watafute namna ya kuweza kufika na kwenye masikio, tukiweza na huko basi mambo yetu yatakuwa yanakwenda vizuri sana, lakini kabla ya hapo, mwezi huu kabla haujaisha tutaanza mikutano ya taasisi ni katika jitihada za kuhakikisha mnapata taarifa za kutosha,” alisema.
Aidha, alimpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kwa kuandaa mkutano huo wa wahariri na kueleza kuwa, hiyo ni sehemu ya mkakati wa ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali katika kuuhabarisha umma kuhusu maendeleo yanayofanywa na serikali.