Mazingira ya uwekezaji yalipa

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema uwekezaji uliofanywa na kiwanda cha saruji Tanga unaonesha kuna mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.
Aidha, amesema serikali ina dhamira ya kuirudisha Tanga kuwa mkoa wa viwanda kama ilivyokuwa awali.
Rais Samia alisema hayo jana wakati akifungua kiwanda cha chokaa na saruji awamu ya pili cha Maweni kilichopo Tanga wakati akiendelea na ziara yake mkoani humo.
“Sote tunakumbuka Tanga ya zamani, Tanga ya viwanda na iliyokuwa inatupa fahari… kwa bahati mbaya Tanga ya viwanda ilipotea, lakini dhamira ya serikali ni ileile kuirudisha Tanga kuwa Tanga ya viwanda,” alieleza Rais Samia.
Aliongeza: “Uwekezaji walioufanya ni ishara kwamba wana imani na sera zetu za uwekezaji, wana imani na mazingira yetu ya biashara, lakini zaidi wana imani na nguvu kazi yetu hapa”.
Aidha, amesifu uwekezaji uliofanywa na kiwanda hicho cha Maweni.
“Niwapongeze kwa uwekezaji mkubwa walioufanya hapa tangu waanze uzalishaji, wamenipitisha kwenye kiwanda, uwekezaji walioufanya na jinsi wanavyozalisha kufikia tani milioni tatu, huu ni uwekezaji mkubwa,” alisema Rais Samia.
Akizungumzia fursa za ajira ambazo kiwanda hicho kimetoa, Rais Samia amesema kimetoa ajira zaidi ya 800 za moja kwa moja na zile ambazo si za moja kwa moja, akieleza kuwa matarajio yake ni kuwa ajira kiwandani hapo zitaongezeka.
Pia, amehimiza kiwanda hicho kulipa ushuru wa halmashauri na kuendeleza ushirikiano mzuri baina ya halmashauri na kiwanda hicho.
“Ushirikiano wenu na uhusiano wenu mzuri na wawekezaji ndio utakaowafanya walipe vyema tozo na kodi zenu za halmashauri,” alieleza.

Ametoa maagizo kwa wakazi wa Tanga kutumia saruji inayozalishwa katika kiwanda hicho kuboresha makazi yao na kujenga nyumba za kisasa.
“Kiwanda hiki kipo Tanga, kinachozalishwa Tanga lazima kiimarishe na kinawirishe Tanga. Niwaombe sana wana-Tanga tumieni mazao haya saruji inayozalishwa hapa kuboresha makazi yetu, kuboresha nyumba zetu, kujenga nyumba za kisasa ambazo zinakwenda kuipa hadhi zaidi mkoa wetu wa Tanga,” aliagiza Rais Samia.
Aliwataka wafanyakazi waendelee kufanya kazi kwa bidii. “Niwaombe wafanyakazi chapeni kazi, fuateni sheria za kazi, lakini mwajiri afuate sheria za kazi za nchi yetu ili awape ujira mwema watu wetu na yale yote wanayostahiki,” alisema.



