‘Mbunge asipeperushe bendera akiendesha gari mwenyewe’

DODOMA; BUNGE leo Juni 11, 2025 limepitisha mapendekezo ya maboresho ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ambapo miongoni mwa maboresho hayo ni kuweka masharti ya kusimamia upeperushaji wa bendera katika gari la Mbunge.
Mapema leo asubuhi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge, Mussa Azzan, aliwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu Marekebisho au mabadiliko katika Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023.
“Wabunge wanaruhisiwa kupeperusha Bendera ya Bunge katika ofisi zao na katika magari yao binafsi. Kamati imebaini kuwepo kwa changamoto ya matumizi yasiyo sahihi ya bendera yanayosababisha kushusha hadhi na heshima ya Mbunge.
“Hivyo, inapendekezwa kuweka masharti ya kusimamia upeperushaji wa bendera katika gari la Mbunge. Mapendekezo hayo ni ya kumzuia Mbunge kupeperusha bendera akiwa anaendesha gari lake.
“Mbunge kutopeperusha katika gari lake bendera zaidi ya moja kwa wakati mmoja na vilevile kuelekeza kuwa Mbunge anapaswa kupeperusha bendera akiwa ameketi upande wa kushoto wa gari lake likiwa linaendeshwa na dereva,” anasema.
–