Mbunge: Ni makosa kuhamasisha kususia uchaguzi

DODOMA; MBUNGE wa Jimbo la Lupembe (CCM), Edwin Swalle, amesema ni makosa kuzuia uchaguzi au kuhamasisha watu wasishiriki uchaguzi kwa kuwa kushiriki uchaguzi ni haki ya kikatiba kwa kila Mtanzania.
Swalle ameeleza hayo leo Aprili 30 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia kwenye bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2025-26.
“Nataka niiombe Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia wizara hii ya Katiba na Sheria, tunaomba mlinde haki ya sisi Watanzania ambao tupo tayari kupiga kura Oktoba mwaka huu.
“Jana nimeangalia kule Ruvuma, Songea vyama 12 vimekaa vimesema vinashiriki uchaguzi. Na sisi Wananchi wa Lupembe kwa kazi nzuri aliyofanya Mheshimiwa Rais Samia Hassan kwa kuleta maendeleo kwenye maji, shule, ujenzi wa mahakama na barabara, tumejipanga kwenda kupiga kura,” amesema.
Amesema, sio lazima kwa chama ambacho hakitaki kushiriki uchaguzi basi wasubiri uchaguzi ujao wa mwaka 2030. Kama kuna sheria haipo sawa taratibu zipo, waende mahakamani.
“Huwezi kufanya ‘reform’ mabadiliko ya sheria kwa kufanya maandamano mtaani Kariakoo. Huwezi kufanya reform ya sheria kwa kuhamasisha watu wasiende kupiga kura,” amesema Swalle.



