Mchakamchaka nafasi za umeya CCM waanza

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kinafunga pazia la kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya meya, naibu meya na wenyeviti wa halmashauri katika halmashauri mbalimbali nchini kabla ya kuanza vikao vya ndani vya kuwajadili wagombea.

Katibu wa Siasa na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga aliliambia HabariLEO jana kuwa fomu zilianza kutolewa jana na baada ya utaratibu huo kufungwa vitaanza vikao vya ngazi ya wilaya vikifuatiwa na mkoa na baadaye taifa kuwajadili na kuwapitisha wagombea.

Aidha, amesema Novemba 30, 2025 itakuwa ni siku ya kuwapata wagombea wa vyama mbalimbali watakaoshindana katika kuwania nafasi hizo katika halmashauri. Amesema mpaka jana wagombea wa CCM waliendelea kuchukua fomu katika halmashauri mbalimbali kwa ajili ya nafasi hiyo huku akitaja kigezo kikuu kinachotazamwa ni mgombea sharti awe diwani wa kuchaguliwa katika kata. SOMA: Bakwata yatahadharisha chuki, visasi uchaguzi mkuu 2025

Aidha, kuhusu malalamiko yanayoweza kujitokeza kutokana na mchakato huo, amesema  CCM imeweka utaratibu bora wa kuwapata wagombea wake usio na mashaka na kuongeza kuwa kama yatakuwepo malalamiko upo utaratibu mzuri wa kuyashughulikia bila kuleta athari katika chama.

Kwa upande wa Mkoa wa Morogoro, Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Uhuru, Latifa Ganzel ni miongoni mwa waliojitokeza kwenye mtanange huo ambapo anawania nafasi ya naibu meya. Katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Morogoro, Khalid Hossein amesema katika siku ya kwanza wanachama watatu ambao ni madiwani wateule walichukua fomu za kuomba kupata ridhaa ya chama kugombea Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro.

Amewataja waliochukua fomu kwa nafasi ya naibu meya ni Latifa, Mohamed Thabit na Yusuph Magoba. Kwa upande wa umeya waliochukua fomu katika siku ya kwanza walikuwa sita, miongoni mwao ni Hamis Ndwata, Yusuph Magoba na Khalid Matengo.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu ya kugombea, naibu meya wa Manispaa ya Morogoro, Diwani mteule wa Viti Maalumu, Latifa alisema baada ya kulitumikia baraza la madiwani kwa muda wa miaka 10 ameona sasa ni wakati mwafaka wa kugombea nafasi ya naibu meya akilenga kusimamia kuongeza vyanzo vipya vya mapato.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button