Mchengerwa: Mradi wa DMDP utajenga barabara za lami DSM

DAR ES SALAAM: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  Mohamed Mchengerwa amesema Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili utajenga barabara za lami katika Mkoa wa Dar es salaam kilomita 250, kuanzisha mfumo wa udhibiti wa taka ngumu, masoko 18 pamoja na vituo vya mabasi tisa.

Mchengerwa ameyasema hayo leo Februari 20, 2024 jijini Dar es salaam kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa fedha za mradi huo  kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ambapo waliotia saini ni Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Mwigulu Nchemba na Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete.

Akizungumza baada ya kusainiwa mikataba hiyo, Waziri Mchengerwa amesema jiji hilo limekuwa na changamoto ya miundombinu, ikiwamo ya barabara, ambapo awamu ya kwanza ya DMDP iliboresha jumla ya kilometa 207 katika halmashauri tatu zilizokuwa chini ya mradi na imeleta  mabadiliko makubwa.

“Sasa hivi mradi huu utatekelezwa kwenye halmashauri zote za Mkoa wa Dar es salaam kila halmashauri itajengewa barabara za lami,  masoko pamoja na vituo vya mabasi, mradi unaenda kuangalia changamoto ya usimamizi wa taka ngumu katika jiji la Dar es Salaam kwa ujumla wake.”amesema Mchengerwa

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya taka kutochukuliwa kwa wakati na vilevile makandarasi wa kukusanya taka ngumu kuwa na mazingira ambayo sio rafiki kwa kufanya majukumu yao kwa ufanisi, mradi huu unatarajiwa kuboresha miundombinu ya taka ngumu kwa maana ya kuanzia katika ukusanyaji, usafirishaji hadi utunzaji wake katika madampo ya kisasa matatu yanatarajiwa kujengwa chini ya mradi huu,” amesema Mchengerwa.

Kadhalika, amesema kupitia mradi  huo master plan ya mifereji mikubwa ya maji ya mvua itaboreshwa na mifereji muhimu itatambuliwa na itajengewa yenye jumla ya kilometa 90 kwa Dar es Salaam nzima.

“Mradi huu ni ishara kuwa Serikali ina nia thabiti ya kutatua changamoto za miundombinu ya Dar es Salaam na kubadilisha hali ya Jiji letu,” amesema Mchengerwa.

Habari Zifananazo

Back to top button