Mchungaji Tengwa: Kila mtanzania aliombee taifa

MCHUNGAJI wa Kanisa la Huduma ya Uamsho na Matengenezo ya Kiroho, Augustine Tengwa amesema ni jukumu la kila mtanzania kuitunza amani ya nchi, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumz leo jijini Dar es Salaam, mchungaji huyo ambaye aliambatana na wachungaji Alpha Kihamba pamoja na Agness Bruno amesema ni muhimu kutanguliza uzalendo, maslahi ya nchi na kumpa ushirikiano Rais Samia suluhu Hassan.
“Nimepewa maono na Mungu kuwataka Watanzania kuitunza amani. Hivyo ninawaomba nyinyi kama waandishi wa habari mfikishe ujumbe huu kwa kila Mtanzania, na pia ninatoa rai kuliombea taifa la Tanzania hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi,” Tengwa amesema.

Mchungaji Tengwa amesema kuwa atafanya ziara katika mikoa mbalimbali ikiwa ni muendelezo wa kuwasihi wananchi kuiweka Tanzania katika maombi.




