Kinara dawa za kulevya adakwa

alisakwa toka mwaka 2000

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imemkamata kinara wa mtandao wa wafanyabiashara maarufu duniani wa dawa za kulevya na washirika wake watatu.

Mfanyabiashara huyo anajihusisha na dawa aina ya Cocaine ndani na nje ya nchi amekamatwa maeneo ya Boko jijini Dar es Salaam na kwamba alikuwa akisakwa tangu mwaka 2000 huku akijificha kwenye biashara ya kuuza magari.

Akizungumza kwenye ukumbi ofisi za mamlaka hiyo jijijni Dar es Salaam leo Januari 25, 2024 , Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo amesema mbali na kumkamata mfanyabiashara huyo pia wamekamata jumla ya gramu 692.336 za Cocaine zinazowahusisha watuhumiwa watatu katika operesheni maalumu inayoendelea nchini.

“Huyu mfanyabiashara ni mkubwa kwa wiki ana uwezo wa kusafirisha watu 10 maarufu (punda), kwa mwezi anauwezo wa kusafirisha watu 100 wanaume kwa wanawake ambao wanameza dawa na kuzipeleka maeneo mbalimbali duniani, kibaya zaidi anatumia watoto wa maskini kuwabebesha dawa za kulevya na wengi wanafia njiani;

Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, dawa ya kulevya aina ya Cocaine ambayo huzalishwa kwa wingi katika Bara la Amerika Kusini husafirishwa kwa njia ya anga na wabebaji (punda).

Amesema kwa wiki watu hao 10 ambao amekuwa akiwasafirisha, wanaume wana uwezo wa kubeba gramu 300 hadi gramu 1,200 wakati wanawake wanabebeshwa gramu 2,000.

“Punda wake mmoja alikamatwa nchini Msumbiji, akatumikia kifungo amemaliza adhabu anatakiwa kurudi nchini alipaswa amtumie nauli lakini amemtelekeza, mfanyabiashara huyu pia wapo watu wake wengine wamekamatwa katika nchi za India, Pakistan, China na nchi nyingine na kila wanapoulizwa kwa nyakati tofauti nani yupo nyuma ya biashara hii wanamtaja mfanyabiashara huyu,”amesema Lyimo.

Aidha Lyimo amesema washirika wa mfanyabiashara huyo maarufu wa dawa za kulevya wawili wamekamatwa jijini Dar es Salaam na mmoja alikamatwa katika Kijiji cha Shamwengo Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya.

“Mfanyabiashara aliyekamatwa ana mtandao mkubwa wa wabebaji (punda) kutoka nchi mbalimbali ambao huwatumia kama punda kubeba kwa njia ya kumeza, hivyo makosa yake yanaangukia katika uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka, muda wowote atapandishwa kizimbani, tutawaambia na hapo mtamtambua kwa jina, bado kuna wenzake tunawatafuta maana mtandao wake ni mkubwa,”amesema Lyimo.

Habari Zifananazo

Back to top button