ufugaji samaki kwa vizimba waanza Ziwa Tanganyika

SERIKALI imeanza utekelezaji wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Tanganyika baada ya mpango huo kuonesha mafanikio makubwa katika Ziwa Victoria.

Akizungumza leo katika Mwalo wa Kasanga uliopo Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti amesema tayari wizara imeanza kutoa elimu kwa wavuvi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika kabla ya kufikisha vizimba hivyo na mbegu bora za samaki.

Mnyeti amesema kwa sasa serikali imetenga Sh Bilioni 20 kwa ajili uwekaji vizimba katika ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa sababu ufugaji wa samaki unakua kwa kasi maeneo mbalimbali duniani.

Amesema upungufu wa samaki kwenye maji ya asili yakiwemo mabonde, maziwa, mito na bahari umetokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa mazingira, ongezeko la watu na uharibifu wa mazalia ya samaki.

Mnyeti amesema ili kunusuru upungufu wa samaki katika masoko ya ndani na nje ya nchi serikali imeamua kuanza kusambaza vizimba kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika ambavyo vitatolewa kwa mkopo nafuu usio na riba.

Aidha Mnyeti amesema serikali itapumzisha Ziwa Tanganyika shughuli zote za uvuvi kwa kipindi cha miezi mitatu kila mwaka kwa miaka mitatu mfululizo ambapo kwa mwaka huu litafungwa kuanzia Mei 15 hadi 15i Agosti 15, 2024 ili kupisha samaki waweze kuzaliana.

Amesema kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Usimamizi wa Uvuvi endelevu katika ziwa hilo na bonde lake ambapo nchi wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika kwa maana ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokeasia ya Kongo, Tanzania na Zambia zilitia saini mkataba huo Tarehe 9 Mwezi Desemba Mwaka 2021 kwenye mkutano wa 9 wa mawaziri wa nchi hizo.

Amebainisha kuwa kupumzishwa kwa ziwa hilo kutatoa fursa kwa wavuvi kujifunza namna bora ya kufuga samaki pamoja na kuwa na njia nyingine za kujipatia kipato zikiwemo za kufuga mifugo na kilimo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere amesema mpango wa serikali kuhamasisha kufuga samaki kwa njia ya vizimba ni mzuri kwa kuwa wavuvi watapata fursa ya kujifunza namna nyingine ya kuendeleza biashara ya samaki na kwamba mkoa utasimamia utekelezaji huo ili wananchi waendelee kunufaika na mazao ya uvuvi.

Aidha, wamekiri kwamba kwa sasa mazao ya samaki yamepungua kwa kiasi kikubwa katika ziwa hilo na samaki wanaopatikana ni wadogo ambao wanahitaji kubakia ziwani ili kukua.

Habari Zifananazo

Back to top button