Mfuko wa akiba wa Taifa kuanzishwa

DODOMA; SERIKALI imesema katika kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, pamoja na hatua zingine, Mpango wa Mendeleo umeelekeza kuanzisha mfuko wa akiba wa Taifa (National Sovereign Wealth Fund).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof Kitila Mkumbo, ametoa kauli hiyo bungeni leo akiwasilisha nyenzo tatu zitakazowezesha kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Nyenzo hizo ni Mpango Elekezi wa Muda mrefu wa miaka 25 (2026/27 hadi 2050/51), Mpango wa Nne wa Maendeleo wa miaka mitano (2026/27 hadi 2030/31) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2026/27.
“Katika kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, pamoja na hatua zingine, Mpango umeelekeza kuchukua hatua zifuatazo:
“ Kuanzisha mfuko wa akiba wa Taifa (National Sovereign Wealth Fund) ambao chanzo chake kitatokana na sehemu ya mapato itokanayo na maliasili za Taifa kama mafuta, gesi, dhahabu na madini mengine.
“Kuongeza makusanyo ya kodi kufikia uwiano wa asilimia 18 ya pato la Taifa (tax to GDP ratio).
“Kujenga uwezo wa wakandarasi wa ndani ili kuongeza kiwango cha ushiriki wao katika miradi ya ujenzi,” amesema.



