Mfumo wa e-CMS kurahisisha huduma za mahakama
MOROGORO: Ofisi ya wakili mkuu wa serikali [OWMS] imeenza kutumia mfumo wa mashauri wa mahakama wa kielektroniki ili kuongeza matumizi ya Tehama uwazi, uwajibikikaji, upatikanaji wa taarifa kwa haraka na Imani kwa wananchi kuhusu utendaji kazi wa vyombo vinavyotoa haki kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na kaimu Naibu Mkuu wa serikali, Mark Mulwambo wakati akifungua mafunzo elekezi kuhusu mfumo wa kieletroniki wa mashauri ya mahakama kuu ya Tanzania [e-CMS] na utunzaji wa nyaraka serikali ambapo ufunguzi huo umefanyika Morogoro na kusema kuwa OWMS imeona ni muhimu kwa watumishi wake kupata mafunzo ya mfumo huo wa mahakama.
Aidha,Mulwambo amesema mfumo wa e-CMS umefanikisha mambo mbalimbali yakiwemo utoaji wa taarifa kwa wahusika wa shauri kwa kusajiliwa na kupangiwa Jaji au hakimu kwani umetoa mwanya wa kujumuisha taarifa za taasisi nyingine za serikali ili ziweze kutumika kusomana, pia mfumo huo umefanikisha usajili wa namba ya utambuzi wa kesi ambayo haijirudii na kutumiwa na mahakama nyingine.
Kwa upande mwingine Mulwambo amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia ujuzi watakaoupata na kuyafanyia kazi kwa kuzingatia uadilifu na usiri katika utendaji kazi kwa kuwa masjala ya sheria ni ofisi nyeti katika kutunza nyaraka za serikali.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha Masjala ya sheria wa OWMS, Dennice Leornard amesema kuwa mfumo wa mahaka ma wa e-CMS utawawezesha wananchi kupata taarifa na kufuatilia mwenendo wa mashauri mahakamani kwa kupata ujumbe kwenye simu zao mkononi na barua pepe.
Pia, katibu wa sheria wa OWMS, Victoria Kawacha ameshukuru ujenzi wa mfumo wa mahakama wa e-CMS kwa kuwa utarahisisha utendaji kazi na kupunguza muda wa kuandika taarifa za mashauri na nyaraka mbalimbali kwenye mjadala kwa kuwa taarifa zitapatikana kwenye mfumo huo.



