Mfumo wa zabuni kidigitali kuleta ushindani kwa wajasiriamali

DAR ES SALAAM: Sekta binafsi nchini Tanzania inatarajiwa kupata msukumo mkubwa baada ya kuzinduliwa kwa mfumo mpya wa kidigitali wa manunuzi uliobuniwa na kampuni ya WinTender, ambao unalenga kubadilisha namna zabuni zinavyopatikana na kusimamiwa.

Mfumo huo ambao ulizinduliwa katika Maonyesho ya Samia Construction Sector & Exhibition 2025, unatarajiwa kufanya mchakato wa zabuni kuwa wazi zaidi, wenye ufanisi, na wenye ushindani wa haki kwa kuwapatia wasambazaji, watoa huduma, wakandarasi na wazabuni jukwaa la kisasa la kutuma na kushinda zabuni.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa WinTender, Chambua Msanga, alisema mfumo huo ni hatua kubwa katika mageuzi ya sekta ya manunuzi. “WinTender inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa taifa kupitia miradi na huduma mbalimbali. Mfumo huu umebuniwa ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu na kwa ushindani,” alisema.

Chambua aliongeza kwa kusema kwamba dhamira ya mfumo hu oni kuondoa changamoto za kuwasilisha nyaraka za zabuni, ambapo kuna muda zinaweza kuchelewa na kwa kutumia karatasi nyingi.

Mfumo huo wa kidigitali ni muhimu zaidi kwa vijana na wajasiriamali wadogo ambao kwa miaka mingi wamekosa fursa kutokana na kukosa maarifa, taarifa sahihi au mtandao wa kupata nafasi za zabuni.
Mkurugenzi alieleza kuwa WinTender imeweka mkazo mkubwa kwa makundi haya ili kuhakikisha wanashindana kwa usawa.

“Tunatoa mafunzo juu ya namna bora ya kuomba, kushinda na kutimiza zabuni. Zaidi ya hapo, tunakusanya taarifa za zabuni kutoka mashirika mbalimbali na kuziweka sehemu moja ili wajasiriamali wazipate kwa haraka. Kupitia akaunti zao za WinTender, pia wanaweza kuwasiliana moja kwa moja na wataalamu wetu wa manunuzi kwa msaada,” alifafanua.

Mfumo huu pia unatarajiwa kushughulikia changamoto ya uwazi katika manunuzi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa muda mrefu.
Kwa miongo kadhaa, mchakato wa zabuni umekuwa ukihusisha urasimu, ucheleweshaji na wakati mwingine madai ya upendeleo.

Kwa kuhamisha kila hatua kwenda kidigitali, WinTender inalenga kurejesha imani katika mfumo wa manunuzi na kuongeza ushiriki mpana.
Mr Chambua alisema, “Kuanzia tangazo la zabuni, uwasilishaji wa maombi hadi matokeo, kila kitu kinaonekana kwa wazabuni wote. Hii inapunguza mianya ya rushwa, kutoelewana au upendeleo,” alisisitiza.

Mbali na kuongeza uwazi, mfumo huu unatarajiwa kuwa na mchango mpana zaidi katika uchumi kwa kuwezesha makampuni kushiriki miradi mingi zaidi na hivyo kuchochea ajira na ukuaji wa biashara.

“Kwa kuongeza wigo wa zabuni zinazopatikana, WinTender inatoa nafasi kwa makampuni na wajasiriamali kushiriki kwenye miradi mingi zaidi. Hii inaleta ongezeko la ajira kwa wananchi, za muda na za kudumu, huku pia ikichochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati,” alieleza.

Kwa kuzinduliwa kwa mfumo huu, WinTender imejipambanua kama kiunganishi muhimu katika ukuaji wa uchumi, ikiwaleta pamoja wazabuni na taasisi nunuzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button