Mgombea aahidi taa 5,000 barabarani

DAR ES SALAAM: MGOMBEA Udiwani wa Kata ya Kigamboni kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dotto Msawa amesema endapo atapewa ridhaa ya kuongoza kwa mara nyingine, ataweka taa zaidi ya 5,000 barabarani.

Amesema atakamilisha uwekaji wa lami kwenye barabara zote zinazohitajika pamoja na kujenga mifereji ya maji ya mvua kwa ajili ya makazi ya wananchi. Msawa ametoa kauli hiyo juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika kata hiyo.

Amesema tayari ameanza kazi kubwa katika sekta za afya, elimu, barabara na ujenzi wa soko la kisasa, hivyo wananchi wampe tena ridhaa ili aendelee.

“Wananchi, naomba kura zenu za ndiyo. Nikamilishe kazi niliyoianza awamu iliyopita. Mliniamini na nikatekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya CCM, sasa naomba mnirudishe ili nimalizie yale yaliyobaki,” amesema Msawa

Kwa upande wa elimu, Msawa amesema kata hiyo imepata Shule ya Sekondari ya Paul Makonda ambayo inaendelea kuboreshwa kwa kujengwa maabara, vyumba vya madarasa na nyumba za walimu na tayari amewasilisha maombi serikalini kwa ajili ya kujengwa shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita.

Ameongeza kuwa shule nyingi za msingi Kigamboni zina majengo ya chini, hivyo ataanza kujenga Shule ya Msingi Raha Leo kwa mfumo wa ghorofa, na tayari fedha za kuanzia zipo.

Kuhusu afya, amesema alipokuwa anaingia madarakani, kata ilikuwa na zahanati pekee. Hata hivyo, kupitia jitihada zake na Serikali inayoongozwa na dk Samia Suluhu Hassan, wamefanikiwa kujenga Kituo cha Afya Kigamboni chenye hadhi ya nyota tatu ambacho sasa kinatoa huduma zote muhimu za afya.

“Wananchi wenzangu wa Kigamboni, mama Samia anatupenda sana. Ameharakisha maendeleo tangu aingie madarakani na ametupatia fedha nyingi kwa ajili ya afya, elimu na barabara. Tumlipe kwa kumpa kura nyingi za ndiyo, na tumshukuru sana kwa moyo huo,” amesema.

Msawa ameongeza kuwa Kigamboni bado haina soko la kisasa, na endapo atachaguliwa tena, atajenga soko kubwa la kisasa katika eneo la Magengeni kwa Urasa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button