Mgombea aahidi usimamizi bora fedha za serikali

ARUSHA: MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Monduli mkoani Arusha, Joseph Issack maarufu kwa jina la ‘Kadogoo’ amesema atakapochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kipaumbele chake cha kwanza atahakikisha fedha zote zilizotengwa na serikali kwa ajili ya miradi inatekelezwa ipasavyo.
Pia atahakikisha maeneo ya malisho yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya mifugo inasimamiwa kwa maslahi ya wananchi.
Kadogoo alisema hayo leo katika Kata ya Esilalei wilayani Monduli katika ufunguzi wa kampeni ya ubunge wa jimbo hilo yaliyohudhuriwa na mamilioni ya watu na kusema kuwa fedha za miradi zilizotolewa na serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan zinafanya kazi zilizokusudiwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Monduli.

Alisema na kusikitika kuona mamilioni ya fedha yaliyopelekwa Monduli kwa ajili ya miradi bado miradi hiyo inasuasua na kutokana na hali hiyo yeye akichaguliwa kuwa mbunge atahakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na sio vinginevyo kwa faida ya wana Monduli.
Kadogoo ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli alisema kuwa anazijua kikamilifu changamoto zote za vijiji 62, vitongoji 236 vya jimbo hilo na kusema kuwa asilimia 75 ya wakazi wa Monduli ni wafugaji na kipaumbele kingine iwapo atachaguliwa ni kuhakikisha kata saba za jimbo hilo zinajengwa mabwawa kwa ajili ya mifugo na kuhakikisha maeneo yaliyotengwa na serikali kwa malisho yanatekelezwa kwa yeye kusimamia hilo.

Alisema wafugaji wa Monduli wanahitaji maji kwa ajili ya mifugo na matumizi ya nyumbani na pia kuwa na uhakika na mabwawa kwa ajili ya mifugo hilo atalipa kipaumbele kwa ajili ya wafugaji na wakazi wa jhimbo hilo.
Mgombea huyo alizungumzia changamoto ya Ziwa Manyara kati ya wananchi wa Mto wa Mbu na Wizara ya Maliasili na Utalii na kusema kuwa atahakikisha anajenga mahusiano mazuri kati ya wavuvi na Mamlaka zinazosimamia ziwa hilo lengo ni kutaka kila mmoja kufaidi rasilimali za Taifa kuliko ilivyo sasa.
Awali mgeni rasmi katika uzinduzi wa Kampeni hiyo,Katibu wa NEC Oganizetion ya CCM Taifa,Issah Gavu na alisema na kuwataka wana Monduli kumpa ushirikiano Kadogoo ili aweze kutekeleza maendeleo ya wananchi wa Jimbo hilo kwa kuwa mgombea huyo anatosha na chenji inabaki kwa kuwa anajua vizuri changamoto za Jimbo hilo.
Gavu alisema pamoja na kumpa ushirikiano Kadogoo katika kuleta maendeleo katika Jimbo hilo pia wana Monduli wasisahau kumpa kura Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk Samia Suluhu Hassan kwani amefanya mambo makubwa katika jimbo hilo ikiwemo afya,maji,elimu na barabara hivyo wanastahili kulipa fadhila.
Alisema pamoja na hilo alisema kuwa Ranch zilizopo katika Jimbo la Monduli zinapaswa kupatiwa wawekezaji wa ndani wenye uwezo na wenye uchungu na nchi ili waweze kuziendeleza na serikali iweze kupata faida.



