Mgombea aahidi utatuaji uuzaji ardhi holela

ARUSHA: MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Simanjiro mkoani Arusha, James Ole Millya amesema endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kipaumbele ni uuzwaji holela wa ardhi usiozingatia sheria na umuhimu kwa wananchi.

Millya amesema hayo katika uzinduzi wa kampeni wa Jimbo la Simanjiro katika Mji wa Orkesmet na kuhudhuriwa na maelfu ya watu wakiwemo viongozi mbalimbali wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya matawi, kata, wilaya na mkoa.

Amesema serikali imetenga ardhi kwa ajili ya malisho na kilimo na maeneo mengine kwa ajili ya shughuli za maendeleo lakini kuna viongozi ngazi ya kijiji kwa kushirikiana na watu wasiokuwa waaminifu wanadiriki kuuza kiholela maeneo ya malisho na kilimo bila aibu hilo hatalikubali katika kipindi cha ubunge wake.

Mgombea ubunge huyo alisema Simanjiro inahitaji wawekezaji kwa ajili ya maendeleo lakini wenye kufuata taratibu na sio kutoa ardhi kubwa kwa njia isiyokuwa sahihi hilo halitakubalika katika kipindi cha ubunge wake kwani wataofanya hivyo watachukuliwa hatua.

‘’Nitashirikiana na Baraza la Madiwani kupiga vita uuzwaji holela wa ardhi ya Simanjiro na atakayetaka ardhi kwa ajili ya uwekezaji itambidi afuate sheria na kanuni namna ya kuipata ardhi hiyo na sio kupita njia za panya kupata ardhi, ‘’alisema Millya.

Aidha, alizungumzia changamoto ya barabara na kusema kuwa hakuna mtu asiyejua kuwa wilaya ya Simanjiro hiyo ndio moja ya changamoto kubwa inayosumbua Jimbo hilo na CCM imeweka katika ilani yake kuhakikisha hilo linapatiwa ufumbuzi hivyo atalisimamia kwa kuwa chama chake kimeshaonyesha wazi kuwa ni moja ya agenda katika miaka mitano ijayo.

Mgombea huyo aliwaomba wakazi wa Jimbo la Simanjiro kumpa kura zote za ndio yeye kama mgombea ubunge ,madiwani na mgombea Urais wa CCM Samia Suluhu Hassan ili waweze kushirikiana na kuifanya Simanjiro kuwa na maendeleo zaidi kwani Rais alipeleka fedha nyingi katika Jimbo hilo miaka mitano iliyopita.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Manyara ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kamepni hiyo, Janes Darabe aliwaomba wana Simanjiro kumpa Millya kura zote ili awe Mbunge kwani mgombea huyo ni mchapakazi na asiye na majivuno na mshirikishaji kwa mambo ya maendeleo.

Darabe amesema Millya ni jembe na anahistoria ya uongozi katika ngazi mbalimbali za siasa Mkoani Manyara na Arusha na kutokana na hali hiyo ndio maana Kamati Kuu ya CCM ilirudisha jina lake kwa kuwa wanamjua kuwa ni mtu na nusu katika uongozi hivyo anastahili kuwa Mbunge Simanjiro.

Aliwaomba wana Simanjiro kumpa Millya kura zote ili awe Mbunge wa Simanjiro ili aweze kutekeleza ilani ya CCM yenye miradi mingi ya maendeleo katika Jimbo hilo kwa faida ya wananchi wa Jimbo hilo na pia kumpa kura mgombea urais wa chama tawala Samia Suluhu Hassana na madiwani.

Katika Jimbo hilo lenye kata 18 wagombea udiwani wa CCM wamepita bila kupingwa katika kata zao kwa kuwa hawana wapinzani katika vinyang’anyiro vyao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button