Mgombea urais ADC aahidi satelaiti kuharakisha kesi

CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimeahidi kujenga mifumo ya setalaiti nchi nzima ili kuboresha huduma kwenye sekta mbalimbali. Mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Wilson Mulumbe ametoa ahadi  hiyo wakati wa mikutano ya kampeni wilayani Ilemela mkoani Mwanza juzi.

Mulumbe amesema satelaiti ni muhimu kwa ajili ya kuboreha huduma, zikiwemo za mahakama kwa kutumia kamera kukusanya ushahidi wa matukio, hasa ya uhalifu mitaani. “Na hii itasaidia mashauri kuendeshwa kwa muda mfupi, kwa sababu matukio yanayoshikwa na kamera ni ushahidi unaojitosheleza, kiasi kwamba mtuhumiwa hana jinsi ya kukana kosa,” alisema.

Mulumbe amesema pia satelaiti zitasaidia kuimarisha doria, zikiwemo za kwenye Ziwa Victoria ambako mara kwa mara wavuvi wanadaiwa kuvamiwa na kuporwa.

Amesema satelaiti hizo zitasaidia kugundua rasilimali ardhini, hasa katika sekta ya uziduaji, yakiwemo madini urani yatakayosaidia kuongeza uzalishaji umeme. “Hakuna sababu ya mgao au kukatika kwa umeme katika nchi yetu. Malighafi za kuzalisha tunazo za kutosha, ni suala tu la kuwa na teknolojia za kisasa kuongeza uzalishaji na usambazaji,” alisema Mulumbe.

Pia, Mulumbe amesema serikali ya chama hicho itafunga mitambo ya nishati safi, hasa umeme wa jua na wa upepo katika mikoa yote yenye changamoto ya ukame. SOMA: ADC yaahidi kuruhusu uraia pacha

Mulumbe ameahidi kufufua na kujenga viwanda vipya mkoani Mwanza, hasa vinavyohusiana na uchakataji wa mazao ya shambani ili kupanua mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo. “Tunaamini Tanzania itakuwa imehama kutoka uchumi wa kati hadi wa juu ifikapo mwaka 2030. Nawasihi mjitokeze siku ya kupiga kura, mchague ADC ili tuweke ahadi zetu zote katika vitendo,” alisema.

Mgombea ubunge ADC Jimbo la Ilemela, Shaban Itutu ameahidi upatikanaji wa mazao ya Ziwa Victoria kwa bei nafuu ili kuimarisha lishe za wananchi. “Nyie ndio mko jirani kabisa na ziwa hili, ni lazima muwe wa kwanza kunufaika na rasilimali zilizomo,” alisema Itutu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button