Miaka 30 ya Beijing: Wanawake wanazuiwa mifumo dume

WANAHARAKATI wa haki za binadamu na masuala ya kijinsia wamesema licha ya kupita miaka 30 tangu Mkutano wa Beijing ulioibua ajenda ya usawa wa kijinsia duniani, bado mifumo ya kisiasa na kijamii nchini haijabadilika vya kutosha ili kuwapa wanawake nafasi sawa na wanaume.
Wakizungumza katika mkutano wa International Democracy Day ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, wanaharakati hao walisema jamii na mifumo ya kisiasa bado inawanyima wanawake nafasi ya kuonesha uwezo wao.
Mwanaharakati mkongwe, Dk. Helen Kijo Bisimba, amesema baada ya mkutano wa Beijing sauti za wanawake zilianza kusikika kwa nguvu, lakini mfumo wa viti maalum umekuwa kikwazo badala ya suluhisho.
“Viti maalum vilipangwa kusaidia wanawake waliokosa nafasi katika mfumo, lakini sasa vimekuwa tatizo. Wanawake wana uwezo wa kugombea nafasi za kawaida wanakatishwa tamaa kwa kuambiwa nafasi zao ni viti maalum na kuachia wanaume wagombee,” amesema Dk. Bisimba.
Ameongeza kuwa mila na desturi bado zinawabana wanawake, huku baadhi wakidharauliwa au kuambiwa kazi yao ni kulea watoto. “Mfumo haujawawezesha wanawake kufikia malengo yao, mwanamke akikosea analawumiwa zaidi kuliko mwanaume,” amesema.
Kwa upande wake, Dk. Ananilea Nkya, mwanaharakati na mwandishi wa habari, alisema mkutano wa Beijing uliwaongezea nguvu wanawake siyo tu kwenye uongozi, bali hata kwenye kilimo na biashara.
“Tanzania ilinufaika zaidi kwa sababu mkutano ule uliongozwa na Mtanzania, Getrude Mongella. Kwa mara ya kwanza tuliona bajeti ya serikali ikitengenezwa kwa mrengo wa kijinsia, ikilenga vijana, wanawake na wazee,” amesema Dk. Nkya.
Mwanaharakati Deus Kibamba alisema mchango wa wanaume haupaswi kuachwa nyuma katika mapambano ya usawa wa kijinsia.
“Mfumo dume unawanufaisha wanaume, lakini pia kuna wanawake wachache wananufaika nao. Shida ni ukosefu wa utashi wa kisiasa. Usawa wa kijinsia si ajenda ya wanawake pekee, ni jukumu letu sote, kuanzia katika malezi ya watoto wa kike na wa kiume,” amesema Kibamba.
Naye Dk. Consolata Sulley, amesema akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi wakati wa mkutano wa Beijing aliona mabadiliko makubwa ya fikra katika jamii.
“Kuanzia 1992 hadi 2010 tuliona hali ikibadilika, hasa tulipoanza kujadili elimu ya uraia chuoni. Hata hayati Benjamin Mkapa aliwahi kusema changamoto kubwa ni elimu ya uraia. Kama hatutabadili utamaduni wa kisiasa, tutabaki kupiga kelele bila matokeo,” amesema.