Miji mikongwe; Fahari inayoitambulisha Tanzania kimataifa

TANZANIA ni nchi iliyobarikiwa vivutio vingi tofauti ikiwemo wanyamapori, mali kale, utamaduni, misitu, milima na fukwe za bahari.
Mbali na kuwa vivutio vya wanyamapori vimechukua nafasi kubwa kwa kujulikana, vipo vivutio vingine kama misitu na maeneo ya mali kale ambayo mengine yamepata nafasi ya kuwa katika orodha ya urithi wa dunia.
Miongoni mwa maeneo ya mali kale ambayo yanaipa fahari Tanzania na kuifanya itambulike kwa namna ya kipekee ni pamoja na maeneo ya miji mikongwe na miji ya kale. Makala hii itaangazia maeneo ya kale yanayopatikana Tanzania, sifa na hadithi za kuvutia zilizomo ndani yake.
Mji Mkongwe Zanzibar
Tovuti ya zanzibarkwetu inauelezea Mji Mkongwe, Zanzibar kuwa ni hifadhi ya kimataifa ambayo imeingizwa katika orodha ya urithi wa dunia kutokana na kuwa na majengo yanayoelezwa kuwa ni ya kale yaliyojengwa kabla ya Karne ya 19.
Eneo hilo lina ukubwa wa hekta za mraba 125 na majengo yake yakiakisi ujenzi wa India, Afrika na Ulaya. Mwaka 2000 mji huo uliingizwa rasmi katika orodha ya urithi wa dunia ikiwa ni baada ya tathmini ya kimazingira na kuandaliwa kwa mpango mkakati wa kuendeleza uhifadhi wa mji huo.
Tovuti hiyo inabainisha kuwa moja ya vigezo vya mji huo kuingia katika orodha hiyo ni mwingiliano wa makabila kwa kile kilichoelezwa kuwa watu wa eneo hilo wana asili na utamaduni wa kuishi pamoja kwa muda mrefu bila kubaguana.
Vigezo vingine ni ushirikiano wa kibiashara baina ya Zanzibar na Asia na historia ya biashara ya utumwa. Inaelezwa mji huo ni hazina kubwa kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba sanjari na wageni wanaofika visiwani humo kwa kuwa ni moja ya maeneo muhimu yanayotembelewa ili kujua historia mbalimbali na tamaduni.
Mji Mkongwe Mikindani
Mikindani ni moja ya miji mikongwe inayopatikana katika pwani ya Afrika Mashariki, ulioanzishwa na jamii ya wenyeji takribani miaka 200 kabla ya Kristo. Meneja Mafunzo katika Hoteli ya Mafunzo ya Old Boma, Mji Mkongwe Mikindani, Lucas Navilongo anapoelezea kuhusu historia ya mji huo anasema ulianza kupata umaarufu tangu wakati huo kwa kuwa ndiyo mji wa kwanza kuendelea kabla ya Mtwara Mjini.
“Wakati huo tunazungumzia mji wa Mikindani ukiwa unatambulika kama Kimbuli ama Chimbuli,” anasema. Anaongeza: “Hapo ni wakati wa makabila ya wenyeji ambao walikuwa wakiishi kwa kuhama, tunazungumzia watu kutoka Msumbiji ambao ndiyo hao akina Chimbuli.
“Wakaishi Mikindani miaka mingi iliyopita. Walipoishi hapa, wakafanya jina la mji huu kupitia jina la ule ukoo maarufu wa Chimbuli waliohama kutoka Msumbiji wakafanya huu mji ujipatie umaarufu wa jina la Chimbuli,” anasema.
Kuhusu kubadilika Navilongo anasema ziko nadharia tatu tofauti lakini moja iliyokubalika inaeleza kuwa mji huo ulibadilisha jina kuwa Mikindani kutokana na asili yake ya kuwa na mashamba ya minazi. Anasema eneo hilo lilikuwa limepandwa minazi ambayo ilikuwa bado midogo kwa hivyo watu walikuwa wakiita minazi mikinda (minazi midogo) na ndipo jina la Mikindani lilipoibuka likimaanisha kwenye minazi mikinda.
Mji huo umebeba hadithi nyingi ikiwemo historia ya utawala wa Wajerumani, safari ya David Livingstone na juhudi zake za kukomesha biashara ya utumwa kusini na historia ya biashara ya watumwa yenyewe. Katika mji huo bado yapo majengo mbalimbali ya kale ambayo mengine bado yanatumika kwa makazi na shughuli nyingine na ni kivutio kizuri kwa wanaotembelea mji huo.
Kilwa Kisiwani
Huu ni mji wa kale unaopatikana Kusini mwa Tanzania, kilometa moja kutoka mji wa Kilwa Masoko, Makao Makuu ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi. Ni moja ya miji iliyobarikiwa kuwa na mabaki ya magofu na majengo ya kale yenye hadithi za kuvutia zinazokaribisha watalii katika kisiwa hicho.
Kutokana na umuhimu wa historia inayobebwa na mji huo, mwaka 1981 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliuingiza mji huo katika Orodha ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia. Mwongoza watalii katika mji wa Kilwa Masoko, Daudi Gidion anaelezea kuwa historia ya mji huo ilianza katika karne ya tisa mji huo ulipoanzishwa na Wamwera chini ya kiongozi wao anayetajwa kwa jina la Mnimbo.
Baadaye karne hiyo hiyo, Washirazi waliingia kutoka Iraq na kumlaghai Mnimbo ambaye alikubali kuuza kisiwa hicho na kuwaachia Washirazi eneo hilo. “Baadaye Kilwa Kisiwani ilibadilika na kuwa lango la biashara kwa kuwa washirazi walikuwa wafanyabiashara,” anasema Daudi.
Washirazi waliubadilisha mji huo na kuufanya kuwa mji wa biashara Afrika Mashariki uliokutanisha wafanyabiashara kutoka nchi za Asia kama China, India pamoja na Australia. Mji huo pia una historia muhimu ya
kuwa mji wa kwanza kumiliki sarafu yake wenyewe Afrika Mashariki katika Karne ya 12.
Ni katika mji huo kuna misikiti ya kale, gereza la Wareno ambalo sasa linatumika kama makumbusho ya mji huo, magofu na makaburi ya kale. Songo Mnara Ni safari ya takribani saa moja kwa boti kutoka mji wa Kilwa Masoko (Makao Makuu ya Wilaya ya Kilwa) hadi kilipo kisiwa hicho (Songo Mnara) chenye utajiri wa historia ya magofu ya kale.
Kisiwa hicho pia kiko katika Orodha ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia unaotambuliwa na UNESCO. Historia ya kisiwa hicho inaanzia katika Karne ya 15, Washirazi wakiongozwa na Sultani Ali bin Ibrahim walipoingia na kufanya biashara kisiwani humo kama ilivyokuwa kwa Washirazi wa Kilwa Kisiwani.
“Karne ya 16 Kisiwani ilipovamiwa na Wareno, Washirazi wengi walihamia Songo Mnara kutokana na Wareno kuharibu biashara Kilwa Kisiwani,” anasema Gidion. Historia inaeleza kuwa Washirazi waliendelea na biashara mpaka Waingereza walipoingia Songo Mnara na kuweka makazi hadi pale Tanganyika ilipopata uhuru na kisiwa hicho kuwa huru pia.
Kama ilivyo kisiwani, Songo Mnara pia kina utajiri wa magofu na makaburi ya kale yaliyobeba hadithi za kuvutia za watawala wa Kiarabu na maisha yao na wasaidizi na wenyeji wa mji huo.
Mji Mkongwe Bagamoyo
Mji Mkongwe wa Bagamoyo au Mji Mkongwe kama unavyojulikana na wenyeji, uko Mashariki mwa Tanzania kando ya Bahari ya Hindi, Mkoa wa Pwani. Ni mji ambao una majengo ya kale ya kihistoria, ambayo yalitumiwa na utawala wa kikoloni wa Wajerumani katika Karne ya 18 na 19 kwa shughuli mbalimbali.
Pia, yamo majengo yaliyotumiwa na utawala wa Waarabu ikiwemo jengo la Ngome Kongwe lililojengwa mwaka 1897. Majengo hayo yanajumuisha pia makao makuu ya utawala wa Wajerumani, soko la watumwa, nyumba ya forodha ya Wajerumani na gereza la nyumba ya watumwa.
Mbali na majengo ya kale mji huo unapambwa na mandhari nzuri ya Bahari ya Hindi. Mji huo umebeba hadithi mbalimbali za kuvutia ambazo mtu atazifurahia anapotembelea.
Mji wa Kilwa Kivinje
Kivinje ni mji mdogo ulio pembezoni mwa Bahari ya Hindi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi. Kama ilivyo ikwa miji mingine ya kale mji huo nao unazo hadithi zake sambamba na magofu ya kale. Tofauti ya Kivinje na Kisiwani au Songo Mnara ni kuwa magofu yake yako katikati ya mji na mengine yakiendelea kutumika kwa makazi kama ilivyo kwa Mji Mkongwe Mikindani mkoani Mtwara.
Kwa mujibu wa historia, wakati wa utawala wa Zanzibar, Kivinje ilikuwa makao ya liwali wa Sultani kwa Pwani ya Kusini na bandari yake ilikuwa muhimu katika biashara ya utumwa na kulifanya eneo hilo kuwa lango kuu la biashara ya utumwa katika eneo la Kusini.
Tovuti ya ‘tanzaniatourism’ inaeleza kuwa makadirio ya watumwa walioingia Kivinje kwa mwaka ilikuwa ni watumwa 20,000 wakitokea maeneo mbalimbali ya kusini kabla ya kusafirishwa kwenda katika masoko makuu ya Zanzibar na Bagamoyo.
Mkazi wa Kilwa Kivinje, Mohamed Mgombela anaelezea kuwa Kilwa Kivinje ina utajiri wa mali kale za historia zinazoweza kuvutia wageni hasa watafiti na wanahistoria.