Mil 120/- zafidia wafanyabiashara Soko la Mashine Tatu Iringa

IRINGA: Wafanyabiashara 40 wa Soko la Mashine Tatu, mjini Iringa, waliopoteza bidhaa na mitaji kufuatia ajali ya moto, wamekabidhiwa hundi ya Sh Milioni 120 kama fidia kutoka Kampuni ya Bima ya Reliance Insurance kwa kushirikiana na Benki ya NMB.

Hatua hiyo inalenga kuwasaidia kurejesha mitaji na kuendeleza biashara zao, huku wafanyabiashara wengine wakihimizwa kujiunga na bima ili kujikinga na majanga kama hayo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo katika Soko la Mlandege, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk Baghayo Saqware, alisema tukio hilo ni mfano halisi wa faida za bima kwa wafanyabiashara.

Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mfanyabiashara kulinda mali zake kwa kukata bima, kwani majanga hayatabiriki.

“Elimu ya bima ni muhimu sana. Wafanyabiashara wengi huzingatia shughuli za kila siku bila kujiandaa kujikinga na majanga. Ni wakati sasa wa kubadili mtazamo,” alisema Dk Saqware.

Ravi Shankar, Mkurugenzi Mtendaji wa Reliance Insurance, aliwashukuru wafanyabiashara kwa mshikamano waliouonyesha baada ya tukio la moto, akisema kampuni yake itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara wa Iringa.

SOMA  ZAIDI

 Biashara Mashine Tatu Iringa zageuka majivu

“Bima si gharama bali ni uwekezaji wa usalama wa biashara. Wafanyabiashara wasikate tamaa, waendelee kuamini huduma za bima,” alisisitiza Shankar.

Afisa Biashara wa Mkoa wa Iringa, Asifiwe Mwakibete, alizipongeza Reliance Insurance na NMB kwa mshikamano wao, akisema tukio hilo limewafungua macho wafanyabiashara wengi kuhusu thamani ya bima.

“Mara nyingi wafanyabiashara hutambua umuhimu wa bima pale majanga yanapowapata. Ni vyema kujiandaa mapema. Waliopokea fidia hii wawe mabalozi wa kuhamasisha wengine,” alisema Asifiwe.

Mwenyekiti wa Umoja wa Masoko wa Manispaa ya Iringa, Rafael Ngulo, alikiri kuwa fidia hiyo imeleta faraja kubwa kwa waathirika.

“Wengi walikuwa kwenye hali ngumu baada ya kuunguliwa bidhaa na mitaji. Mshikamano wa NMB na Reliance ni mfano wa kuigwa,” alisema Ngulo.

Kwa upande wake, Martin Masawe, Mkuu wa Idara ya Bima NMB, alibainisha kuwa mchakato wa madai uliendeshwa kwa urahisi na bila usumbufu, jambo lililoongeza imani kwa wateja.

“Bima za biashara huanzia Shilingi 10,000 pekee na zinaweza kulipa fidia hadi Sh 500,000. Ni nafuu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati,” alifafanua Masawe, akiahidi kuendelea kutoa elimu ya kifedha na kuhamasisha mikopo ya kuongeza mitaji.

Baadhi ya wafanyabiashara waliopokea hundi walieleza kuwa msaada huo umewapa ujasiri wa kurejea sokoni.

“Fidia hii imeniinua. Nimepata nguvu ya kuanza upya biashara. Wenzangu wasikate tamaa, waamini bima,” alisema Maria Ngoda, mfanyabiashara wa bidhaa mbichi katika Soko la Mlandege.

Kwa pamoja, wafanyabiashara hao waliishukuru Reliance Insurance na NMB kwa msaada na mshikamano waliouonyesha, huku wakiahidi kuhamasisha wenzao katika masoko yote ya Iringa kujiunga na bima.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I get paid over 220 Bucks per hour working from home with 2 kids at home. i never thought i’d be able to do it but my best friend earns over 15k a month doing this and she convinced me to try. the potential with this is endless…,

    COPY HERE➤➤ https://work99.site

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button