Mil 555 zatolewa mkopo kwa wajasiriamali Kigoma Ujiji

BENKI ya CRDB imetoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 555.6 kwa vikundi 58 vya wajasiliamali kutoka makundi maalum katika manispaa ya Kigoma Ujiji ili kuwezesha wajasiliamali hao kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji, Jabiri Majira akizunguma wakati Mkuu wa wilaya Kigoma, Dk.Rashid Chuachua akikabidhi hundi kwa vikundi hivyo amesema kuwa fedha hizo zimetolewa kwa vikundi hivyo kutoka mapato ya ndani ya halmashauri kupitia Program ya mikopo ya Benki ya CRDB maarufu kama imbeju.

Mkuu wa wilaya Kigoma Dk Rashid Chuachua.

Majira amesema kuwa kutolewa kwa mikopo hiyo ni muendelezo wa halmashauri hiyo kutoa mikopo kwa makundi maalum ili kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutoa mikopo kwa makundi hayo kuwezesha kuimarisha shughuli zao za uchumi na biashara kuwa na tija na kwamba kwa mwaka huu pekee tayari zaidi ya sh milioni 600 zimetolewa.

Afisa Ruzuku wa Benki ya CRDB Makao Makuu, Baraka Kayila amesema kuwa kupitia benki ya hiyo katika program yake ya imbeju CRDB inatoa mikopo kwa wajasiliamali kutoka katika mapato ya ndani ya halmashauri ili kutekeleza agizo la serikali la halmashauri kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato yake ya ndani.

Amesema kuwa utaratibu huu unaanza na mafunzo kwa wajasiliamali ya uandishi wa maandiko ya biashara, usimamizi wa biashara, usimamizi wa fedha, usimamizi wa rasilimali watu na utafutaji wa masomo mambo ambayo yakisimamiwa wajasiliamali watafanya vizuri kwenye biashara zao na kuweza kurejesha mikopo.

Mkuu wa wilaya Kigoma, Dk Rashid Chuachua amesema kutolewa kwa mikopo hiyo kumekuwa na tija kubwa kwa wajasiliamali wadogo kufanya shughuli zao kwani wengi wao shughuli zao zilidumaa kwa kukosa fedha za kutekeleza mambo ambayo yanazipa uhai biashara hizo ikiwemo masoko.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button