Millen Magese jaji mkuu Tamasha la Mavazi Samia

MWANAMITINDO wa Kimataifa Millen Happiness Magese ametangazwa kuwa Jaji Mkuu wa Tamasha la Samia Fashion litakalofanyika Novemba 30 mwaka huu Visiwani Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo baada ya kutangazwa kuwa Jaji Mkuu wa tamasha hilo, Magese amesema ni heshima kubwa kwake kusimama kama Jaji Mkuu wa Samia Fashion Festival, anajivunia kushuhudia wakati huu wa kihistoria ambao unasherehekea ubunifu, stara, na urithi wa kipekee wa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kwa zaidi ya miaka ishirini, nimejitolea maisha yangu katika sekta ya mitindo, urembo, nimezunguka duniani, nikifanya kazi na chapa kubwa na maarufu, nimeona jinsi mitindo inavyothaminiwa katika nchi za ulaya na mataifa mengine, si tu kama sanaa bali kama alama ya utambulisho, urithi, na fahari.
“Niliposikia kuhusu mpango huu wa kipekee, sikusita, nilichukua ndege haraka kuja nyumbani kuwa sehemu ya safari hii ya kihistoria, kwa Tamasha hili si tu kuhusu mavazi; ni kuhusu heshima yetu kama Watanzania,”amesema.
Mwanamitindo huyo ambaye anaishi nchini Marekani kwa sasa amesema tamasha hilo ambalo litapambwa na vazi la Samia ni alama ya stara, uongozi, na heshima ni zaidi ya mavazi ya kawaida. Ni kazi ya sanaa inayostahili kuhifadhiwa katika makumbusho kwa vizazi vijavyo, kama heshima kwa urithi wa kiongozi huyo.
Amesema ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi kuona Vazi la Samia linakuwa ishara ya kitaifa na kimataifa, chanzo cha fahari kinachowakilisha uzuri, nguvu, na umoja wa Tanzania.
“Tukubaliane kufanya kitu cha kipekee, kitu kitakachotupeleka ulimwenguni na kuacha alama katika historia. Kwa wabunifu, wanamitindo, na wote wanaoshiriki, tambueni kuwa hampo tu katika sehemu ya tamasha, bali mnakuwa sehemu ya historia ya kizazi kitakachovutia dunia. Hebu tufanye wakati huu uwe wa kukumbukwa milele.”
Ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Samia ambaye tangu ameingia madarakani ameendelea kusimama imara kuhakikisha sekta ya utamaduni katika tasnia ya mitindo na urembo inapewa nafasi kubwa katika nchi.
Majaji wengine walioteuliwa ni mwigizaji Idris Sultani, mwanamitindo Khadija Mwanamboka, Kiongozi Jokate Mwegelo, wabunifu na wanamitindo Martin Kadinda, Faraja Nyalandu na Nancy Sumari.
Mwanzilishi na Muandaaji wa Tamasha hilo, Khadija Mwanamboka amesema amewashirikisha wanamitindo mbalimbali na kuungana nao katika tamasha hilo ili kusaidia watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi na saratani.
Kwa upande Mwigizaji maarufu nchini İdris Sultan amesema anajisikia furaha kuwa sehemu ya walioshirikishwa katika eneo la majaji na kueleza umefika wakati kwa Watanzania kutoa nafasi kwa wanawake wenye uwezo ukiwemo uongozi na kusisitiza Rais Samia amekuwa mfano mzuri na wa kuigwa .
Pia, amemuomba Rais Samia kutoa maelekezo kwa madereva wa serikali waanze kuvaa suti zitakazoitwa Samia Suti badala ya Kaunda Suti ambazo watu wengi hawamfahamu.