Mitaa ya viwanda yaja kila wilaya

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema serikali yake ijayo itaanzisha mitaa ya viwanda katika kila wilaya nchini.

Mgombea Mwenza wa urais kupitia chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi alisema hayo katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkula wilayani Busega mkoani Simiyu alipokuwa akizindua kampeni za Uchaguzi Mkuu kwenye mkoa huo.

Dk Nchimbi alisema viwanda hivyo vitajengwa ili kuhakikisha Tanzania linakuwa taifa linalojitegemea kiuchumi na lenye heshima duniani kupitia mageuzi ya viwanda.

“Tunataka kuona kila kijana anapata nafasi ya ajira, kila wilaya inakuwa na mitaa ya viwanda na kila kaya inanufaika na maendeleo ya kweli. Hii ndiyo dira ya Rais Samia Suluhu Hassan na CCM,” alisema.

Dk Nchimbi alisema katika miaka mitano ijayo Serikali ya CCM itazingatia kuimarisha huduma za kijamii na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Alisema sekta ya afya itaendelea kupewa kipaumbele kwa kujenga vituo vipya vya afya vinne na zahanati mpya nne wilayani Busega.

Katika sekta ya elimu, Dk Nchimbi alisema shule tano za sekondari na shule mbili za msingi zitajengwa wilayani humo na pia madarasa mapya 76 yataongezwa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.

Aidha, alisema mpango wa maji utahakikisha upatikanaji wa huduma vijijini unafikia asilimia 90.

Alisema katika siku 100 za kwanza za serikali mpya, hatua mahususi zitachukuliwa kusaidia matibabu ya magonjwa likiwemo shinikizo la damu na kisukari.

Dk Nchimbi alisema Sh bilioni 200 zimetengwa kusaidia biashara ndogondogo na kurasimisha wajasiriamali wadogo ili wapate mikopo na kukuza mitaji yao.

Alisema katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Busega imenufaika kwa kujengwa hospitali ya wilaya, vituo vinne vya afya, zahanati saba, shule mpya tisa za sekondari na ongezeko la madarasa kutoka 1,043 hadi 1,342.

Kwa upande wa maji, miradi 15 yenye thamani ya Sh bilioni 12 imetekelezwa ukiwemo wa Lamadi-Mkula ambao umewezesha asilimia 72 ya wananchi wapate maji safi na salama.

Katika kilimo, Dk Nchimbi alisema ruzuku ya mbolea na mbegu bora imeongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali, ambapo alizeti imeongezeka kutoka tani 1.2 hadi 5.5 na uzalishaji wa mpunga kufikia kilogramu 14,000 kutoka kilo 3,900 kwa ekari.

Kwa upande wake, Mbunge wa zamani wa Busega, Raphael Chegeni alisema utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa miaka mitano iliyopita ni ushahidi kuwa chama hicho ndicho kinachoweza kuwaletea wananchi maendeleo.

“CCM imetekeleza ilani yake kwa vitendo, tumeyaona matunda ya uongozi wa Samia, ndiyo maana tunasema mitano tena,” alisema Chegeni.

Mmoja wa watia nia katika Jimbo la Busega, Francis Nanai aliwataka wanaCCM kuungana bila makundi na kumuunga mkono mgombea ubunge wa jimbo hilo pamoja na wagombea wote wa chama hicho.

“Tumeshiriki mchakato, tumeona waliochaguliwa kupeperusha bendera ya chama. Sisi tulioshiriki lakini hatukupata fursa ya kugombea, bado tunasema tunakipenda chama chetu na tunamuunga mkono Samia,” alisema Nanai.

Katika mkutano huo, viongozi na wananchi walimsifu Rais Samia kwa kuonesha dira ya maendeleo na mshikamano wa taifa.

Walisema kiongozi huyo ni kielelezo cha uthubutu na mwakilishi wa heshima wa wanawake nchini.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I just got paid $22k working off my laptop this month!** And if you think that’s cool, my divorced friend has twin toddlers and made over $22620 her first month. details on this website**Want the secret?** Copy this Website and choose HOME TECH OR MEDIA……..

    Here is I started_______ https://Www.CashHive1.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button