“Miundombinu ya barabara iboreshwe kuepusha msongamano”

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa wiki mbili kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Tarura, Tanroads, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), na Kampuni ya BRAVO kushughulikia ubovu wa barabara inayotumiwa na malori kuingia kwenye Bandari Kavu ya Ubungo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake kwenye bandari hiyo kavu, Chalamila amesema msongamano wa malori unaosababishwa na ubovu wa barabara hiyo unahitaji kutatuliwa haraka ili kuendana na ongezeko la mizigo linalotokana na uwekezaji unaofanywa na serikali katika bandari ya Dar es Salaam.

“Ongezeko la mizigo kwenye bandari yetu ni hatua kubwa ya maendeleo, lakini tunapaswa kuhakikisha miundombinu ya barabara inaboreshwa ili kuepusha msongamano. Ninatoa muda wa wiki mbili barabara hii iwe imerekebishwa,” amesema Chalamila.

Advertisement

Aidha, alizitaka TPA na kampuni ya BRAVO kuimarisha mifumo ya upakiaji na ushushaji wa mizigo kwenye bandari hiyo pamoja na kuongeza idadi ya wafanyakazi. Pia alielekeza kuwepo na utaratibu wa malori kupaki nje ya mji kabla ya kufika bandari kavu ili kupunguza msongamano wa magari jijini.

Kwa upande wao, Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Obedi Galus, Mtendaji Mkuu wa kampuni ya BRAVO, Bosco Haule, Kaimu Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam, Paul Mwele, na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Japhari Nyaigeaha, waliahidi kushughulikia changamoto hiyo kwa haraka.

Baadhi ya madereva wa malori, akiwemo Jafari Abdallah na Ramadhani Lugome, walieleza changamoto wanazokumbana nazo kutokana na ubovu wa barabara hiyo, huku wakisema ucheleweshaji wa mizigo umekuwa ukiathiri shughuli zao.

Hii ni hatua muhimu inayolenga kuboresha huduma za bandari kavu ya Ubungo na kupunguza changamoto za usafirishaji jijini Dar es Salaam.