Usafirishaji mizigo bandari ya Mtwara waongezeka

MTWARA : UKUAJI wa Bandari ya Mtwara katika kusafirisha mizigo umeongezeka  kwa asilimia 49 kwa mwaka kuanzia mwaka 2023/2024 kulinganisha na miaka ya nyuma. Meneja wa Bandari ya Mtwara Ferdinand Nyathi amesema hayo leo katika mkutano wa wadau wa Bandari hiyo ambao unaendelea hapa Mkoani Mtwara.

Amesema kwa mwaka 2023/2024 Bandari ya Mtwara ilisafirisha mizigo tani milioni 1.7 na mwaka 2024/2025 ilisafirisha mizigo tani 2.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 49 kwa ukuaji.Amesema matokeo hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa ambao serikali imefanya ikiwemo ununuzi wa vifaa vya usafirisha na kuongeza ufanisi wa kuhudumia shehena. SOMA: Bandari yachangia 40% Pato la Taifa

Akizungumzia mkutano, Nyathi amesema Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) imeandaa mkutano huo wa wadau Mkoani Mtwara kujadili fursa ambazo zinapatikana katika ukanda wa kusini katika kusafirisha mizigo kupitia Bandari ya Mtwara.”Leo tarehe 29 mwezi Septemba, mamlaka ya Bandari imeandaa mkutano mkubwa wa wadau kujadili fursa zilizopo katika mkoa wa Mtwara katika kusafirisha mizigo kupitia Bandari ya Mtwara.

Mkutano huu umewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, mawakala wa meli, forodha na wafanyabiashara kutoka mikoa yote nchini na nje ya nchi,” amesema. Nyathi amesema kupitia mkutano huo, mamlaka ya Bandari itaonyesha jinsi ambavyo Bandari ya Mtwara imejipanga kuhudumia shehena ya korosho ambayo itasafirishwa kupitia Bandari hiyo.

Amesema mkutano huo hufanyika kila mwaka kuelekea ufunguzi wa msimu wa korosho, kuonyesha fursa na ufanisi wa bandari katika kuhudumia shehena ya korosho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button