Mkakati nishati safi ya kupikia wapata mafanikio makubwa

TANGA; WIZARA ya Nishati imesema Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia umekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alisema hayo Muheza mkoani Tanga jana kwenye uzinduzi wa usambazaji mitungi ya gesi ya kupikia na majiko banifu kwa bei ya ruzuku.

Kapinga alisema utekelezaji wa mradi jumuishi wa nishati safi ya kupikia umewafikia watu wengi kutokana na kuongezeka kwa ukuaji wa mapato wa kampuni za usambazaji wa gesi za kupikia.

Alisema mafanikio mengine ni ukuaji wa masoko vijijini pamoja na kuongezeka kwa hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hususani umeme kwa sababu matumizi ya umeme yameongezeka nchini.

“Kupitia Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia tunaenda kuanza na mradi kwenye vitongoji 20,000 na tayari serikali imetutafutia fedha takribani Shilingi trilioni 4.3, mwaka huu tumepatiwa Shilingi trilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza kupeleka umeme kwenye vitongoji 9,000,’’ alieleza Kapinga.

Alieleza kuwa katika hafla hiyo, mitungi ya ruzuku 452,445 imetolewa kupitia jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuwekeza kwenye wizara hiyo pamoja na kufanikisha miradi inayotarajiwa kuongeza wigo katika ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Aliongeza katika kuelekea kutimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa mkakati huo, vipo viashiria vilivyoonesha Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutekeleza mkakati huo, ikiwamo mradi huo kuwa wa kimataifa.

Pia, alisema awali kulikuwa na changamoto ya usambazaji wa vituo vya kujazia gesi vijijini, lakini wameshirikisha sekta binafsi zikiwamo benki ili kurahisisha usambazaji wa mitungi kuwawezesha wananchi kujaza kwa urahisi.

Alisema kupitia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliofanyika Januari 27 na 28, mwaka huu mkoani Dar es Salaam, wizara hiyo inatarajia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia hususani kwenye umeme.

 

Aidha, alimshukuru Rais Samia kwa kuwapatia kibali cha kurekebisha Mfuko wa Nishati Vijijini ili waongeze kuhudumia na maeneo ya mjini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button