Mloganzila yatoa uvimbe kwenye pafu kwa tundu dogo

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa mara ya kwanza imefanikiwa kufanya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye pafu la mgonjwa kwa njia ya matundu madogo.
Upasuaji huo wa kwanza umefanywa na madaktari bingwa wazawa wa hospitali ya Muhimbili Upanga na Mloganzila leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya upasuaji huo Mkuu wa Idara ya Upasuaji Dk Eric Muhumba amesema manufaa ya huduma hiyo ni pamoja na mgonjwa kupunguza maumivu wakati na baada ya upasuaji.
“Pia inapunguza muda wa kukaa hospitalini hususani wodi ya uangalizi maalum, mgonjwa kutokuwa na kidonda kikubwa na makovu makubwa.
Amesema wamekuwa wanatoa huduma hizo hapo awali kwa kufungua kifua na kutoa uvimbe hivyo kufanyika kwa upasuaji wa aina hiyo utarahisisha utoaji huduma.
“Mgonjwa anaendelea vizuri, wataalam tunaendelea kumfuatilia kwa karibu” amesema Dk Muhumba.
Dk Muhumba amebainisha kuwa kufanikiwa kwa huduma za ubingwa bobezi zikiwemo za matundu madogo kumetokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya afya ikiwemo kusomesha wataalam, uwepo wa vifaa tiba vya kisasa vya kutolea huduma na mazingira wezeshi na rafiki ya kufanyia kazi.



