Mnada wa kwanza wa korosho wafanyika Tandahimba

MNADA wa kwanza wa zao la korosho umefanyika rasmi leo kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Wilaya za Tandahimba na Newala cha (Tanecu Limited) katika msimu wa mwaka 2023/24, ambapo tani 7752 zimeuzwa.
Akizungunza katika mnada huo uliyofanyika wilayani Tandahimba mkoani Mtwara, Meneja wa Tanecu Mohamed Nassoro amesema kati ya tani hizo 7752 za korosho zilizoingia katika mnada huo, tani 1771 kutoka Newala na tani 5981Tandahimba.
Amesema tani hizo zote zilizoingia hadi sasa zina ubora, huku akiwataka wakulima kuendelea kuwa watulivu wakati zoezi hilo la minada linapoendelea.
Korosho hizo zimeuzwa kwa bei ya juu Sh 2050 na bei ya chini Sh 1950.

Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora kutoka Bodi ya Korosho Tanzania ( CBT), Revelian Ngaiza amewasisitiza wakulima wa zao hilo kuendelea kuzingatia suala la ubora wa korosho, ili kilinda kile walichokipata kiweze kufika sokoni kikiwa na viwango vinavyostahili.
Mkulima wa korosho kutoka Kijiji cha Naputa wilayani Tandahimba, Subiri Mohamedi amesema:”Tumeuza korosho zetu leo kwa bei ya juu Sh 2050 ya chini Sh 1950, bei tumeridhia kwa sababu tukisema tusubiri mwisho wa siku wanunuzi ni wale wale, mwisho tutauza kwa bei tofauti na hii.”



