DAR-ES-SALAAM: TAASISI ya Miriam Odemba Foundation MOT imemkabidhi ubalozi mbunifu wa mavazi Anjali Borkhataria kwa lengo kuendelea kuithamini jamii ya kitanzania wakiwemo wasichana.
Akizungumza na HabariLEO kutoka nchini Ufaransa, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Miriam Odemba amesema nidhamu, uwakilishi wake mzuri kwa wasichana, ni sababu ya kufanya maamuzi ya kumpa ubalozi mbunifu huyo.
“Tunaamini katika mtoto wa kike, na Anjali ni chachu nzuri kwa binti wa Kitanzania, kuwa nidhamu, bidii na kuishi katika ndoto jambo linalowezekana katika jamii yetu, wapo wengine vijijini, mikoani na maeneo mengine ulimwenguni,” amesema Miriam.
SOMA:https://habarileo.co.tz/mtanzania-aweka-rekodi-ufaransa/
Ameongeza kuwa matarajio kwa balozi wake mpya ni makubwa kama ambavyo aliishi kwenye ndoto zake ni chachu na hamasa kwa mabinti kuziishi ndoto zao.
Kwa upande wake balozi mpya wa taasisi hiyo, Anjali Borkhataria amesema baada ya kupewa ubalozi huo amedhamiria kuanzisha kituo cha mafunzo ambapo vijana watapata nafasi ya kujifunza sanaa kama vile uanamitindo, mitindo, kushona na muziki na kutengeneza maisha yao ya baadaye,”
“Kwa kutoa elimu ya sanaa, tunaweza kumwezesha hata mtoto wa miaka 5 kutambua kwamba anaweza kufikia mambo makubwa. Kila mtoto atapata fursa ya kuendeleza kipani chake, na kuwatia moyo kuwa na ndoto kubwa na kuamini uwezo wao,” amesema Anjali.SOMA: https://www.miriam-odemba-foundation.org/
Juni 25, 2024 mbunifu huyo aliiheshimisha nchi baada ya kuwa mbunifu wa kwanza kutumbuiza kwenye onesho la ‘pop-up’, lililoandaliwa na Galeries Lafayette nchini Ufaransa, lakini anajiandaa kumvisha Rais Samia Suluhu Hassan vazi maalum litakalokuwa na nakshi za Kiswahili likielezea asili na tamaduni za Kitanzania.