MOI yajivunia kupata mafanikio makubwa

DAR ES SALAAM; Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), imeeleza mafanikio waliyoyapata kutoka Februari hadi Mei 2025 ambapo jumla ya wagonjwa 77,147 walipatiwa huduma za matibabu huku wagonjwa 73,887 wakiwa ni wa nje na 3,262 walilazwa.

Taarifa iliyotolea kwa vyombo vya habari leo na Meneja Uhusiano, Patrick Mvungi imesema katika kipindi hicho zaidi ya wagonjwa 2,300 walifanyiwa upasuaji wa kibingwa na bobezi, wagonjwa 984 walipata upasuaji wa kibingwa na 2,046 walipata upasuaji wa kawaida.

“MOI inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kawaida ya kutoa huduma bora ya matibabu na matibabu ya kibingwa kwa Watanzania na raia wa nchi jirani, idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa uchunguzi wa radiolojia katika kipindi hicho ni 28,030 na uchunguzi huo ni pamoja na X-ray, CT-San, MRI na huduma nyingine za radiolojia,” amesema Mvungi.

Mvungi ameeleza kuwa katika kipindi hicho jumla ya wagonjwa 26 walipata upasuaji na uchunguzi wa mshipa wa damu kwenye ubongo bila kufungua fuvu katika maabara ya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu la kichwa (Angio Suit).

Pia Mvungi amesema wagonjwa 1,299 walipata huduma katika kliniki ya MOI kwa ajili ya huduma wagonjwa maalum na wa kimataifa na katika kipindi hicho jumla ya wagonjwa 813 walipatiwa msamaha wa matibabu.

“Pamoja na mambo mengine, MOI inaendelea kutekeleza mradi wa kimkakati wa idara mpya ya wagonjwa wa nje (New OPD) na mradi wa X-Tumaini unaoiwezesha MOI kutoa huduma kwa wagonjwa zaidi ya 1,500 kwa siku, ikilinganishwa na 500-700 wanaopata huduma kwa sasa.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button