Mpango asisitiza matumizi bora ya barabara

Makamu wa Rais Philip Mpango akishiriki Ibada katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma.
MAKAMU wa Rais Philip Mpango amewasihi wananchi kutumia vema miundombinu ya barabara inayojengwa na serikali ili kuepusha ajali zinazopelekea madhara makubwa.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akizungumza na waumini mara baada ya kushiriki Ibada katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma.
Amesema ujenzi wa Barabara kiwango cha lami katika maeneo mbalimbali ikiwemo kijijini hapo utongeza  usafiri wa vyombo vya moto hivyo ni muhimu kujifunza na kuwafundisha watoto namna bora ya kutumia barabara hizo.
Aidha Makamu wa Rais amesema ujenzi wa miundombinu ni gharama hivyo wananchi wanapaswa kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewahimiza wananchi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Amesema zoezi hilo ni muhimu kwa kuwa linatoa fursa ya kupata viongozi wanaoishi na wananchi katika maeneo yao.
Amewaasa kuchagua viongozi bora watakaojitolea kushughulikia changamoto za wananchi kuliko maslahi binafsi.