Mpina sasa kugombea urais

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Masijala Kuu Dodoma imeamuru Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutoa fursa kwa mgombea urais kupitia tiketi ya ACT Wazalendo, Luhaga Mpina kurudisha fomu na mchakato wa kupokea uendelee pale ulipoishia Agosti 27, mwaka huu.
Uamuzi huo umetolewa mahakamani hapo na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Abdi Kagomba, Jaji Evaristo Longopa na Jaji John Kahyoza lilipopelekwa kwa ajili ya hukumu.
Katika kesi hiyo walalamikaji ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa ACT Wazalendo na wa pili ni Mpina dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Msingi wa kesi hiyo ilidaiwa kuwa chama hicho kilichukua hatua kutokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa Mpina kuomba kuteuliwa na INEC kuwa mgombea urais wa chama hicho, na wa INEC kumzuia kurejesha fomu yake ya kuomba uteuzi aliyokabidhiwa awali kuijaza.
SOMA: Mpina aenguliwa kugombea urais
Awali, akisoma uamuzi huo, Jaji Kagomba amesema wapeleka maombi waliwasilisha maombi tisa ambayo mahakama iliangalia katika viini vitatu, cha kwanza kikiwa ni iwapo INEC ilivunja Ibara ya 74 (11) ya Katiba ya Tanzania kwa kumzuia Mpina kurudisha fomu.
Waombaji pia waliiomba mahakama itoe tamko kwamba kitendo cha INEC kufanya hivyo baada ya kupokea barua ya msajili ni kupoteza uhuru wake kwa kufuata kifungu tajwa ambacho kinaitaka ifanye kazi na majukumu yake bila kupangiwa na taasisi au chama chochote.
Jaji Kagomba amesema kiini cha pili ni mahakama iangalie kitendo cha INEC kumzuia Mpina kurudisha fomu bila kupewa nafasi ya kusikilizwa kilivunja haki ya msingi ya wapeleka maombi kusikilizwa.
Amesema pia mahakama inaangalia wadaiwa wana haki gani, akizingatia ombi la mpeleka maombi namba mbili la kuitaka INEC kumlipa Sh milioni 100 kama fidia ya athari waliyosababisha kwa Mpina.
Amesema pia wapeleka maombi katika mawasilisho yao walidai zuio lilifanyika kinyume cha sheria kabla ya muda wa kufanya hivyo haujafika, pia waliomba mahakama itoe amri ya kuendelea na mchakato.
Kwa upande wa wajibu maombi ambao ni INEC ulidai ulifanya uamuzi baada ya kubaini mgombea alikuwa hana sifa, hivyo kusema ilipokea maelekezo hayo ni maoni na hisia tu, pia walitupa wenyewe haki yao ya kusikilizwa kwa kutopinga uamuzi wa INEC.
Baada ya hayo, Jaji Kagomba amesema mahakama imeona baada ya kupitia barua iliyotoka kwa msajili hawakuona neno lolote lililokuwa linatoa amri kwa INEC, hivyo mahakama haiwezi kutumia maoni na hisia kufanya maamuzi.
“Na sisi tunaona jaji mwenzetu kwenye kesi tulizotumia kwamba kwa kuwa barua haikutoa maelekezo au amri tunashindwa kuamua kuwa INEC iliamua kwa kufuata yale yaliyoandikwa na Msajili yalikuwa ni maelekezo na si amri hivyo tume ilikuwa na uhuru,” amesema Jaji Kagomba.
Katika suala la walalamikaji kudai kutosikilizwa mahakama ilisema inakubaliana na hilo kuwa maamuzi yalifanywa bila walalamikaji kupewa fursa ya kusikilizwa, INEC ilifanya uamuzi ambao umeathiri waombaji, hivyo ilifanya uamuzi kinyume cha katiba inavyoelekeza.
Kwa kuzingatia hilo, mahakama imetoa amri kwa kuwapa waombaji fursa ya kuwasilisha fomu za mgombea huyo na mchakato wa kuzipokea uendelee pale mchakato ulipoishia Agosti 27, mwaka huu.
Kuhusu gharama, amesema zitabebwa na kila upande, hivyo kuhusu hoja ya muombaji wa pili kulipwa Sh milioni 100 mahakama imelikataa.
Akizungumzia hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele amesema watafuata uamuzi wa mahakama.
“Labda kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali akikata rufaa tutasubiri, lakini kwa sasa tutafuata uamuzi wa mahakama,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Mwenezi Taifa wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo amesema, “Baada ya kupata taarifa
rasmi ya hukumu tutaipeleka tume na wao watatupangia tarehe ya kurudisha fomu kwa mgombea wetu wa urais
na tutaanza kampeni”.



