Mradi EBARR wafikia asilimia 95 Zanzibar

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis.

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumoikolojia Vijijini (EBARR) umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wake kwa upande wa Zanzibar.

Amesema hayo leo Novemba 7 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Tamima Haji Abass aliyetaka kufahamu kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa upande wa Wilaya ya Kaskazini, Unguja.

Naibu Waziri Khamis amesema shilingi bilioni 1.4 zimetumika kutekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo kuandaliwa kwa Mpango wa Matumizi ya Ardhi katika Shehia za Matemwe Kijini, Mbuyutende na Jugakuu ikiwa ni pamoja na uchimbaji na ujenzi wa visima sita na ujenzi wa vitalu nyumba (greenhouse) vitatu kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga.

Advertisement

SOMA: EBARR yasaidia upimaji mipaka Simanjiro

Ametaja shughuli zingine kuwa ni ununuzi wa boti sita za kisasa na vifaa vya uvuvi, ujenzi wa vituo vitatu vya ufugaji, utengenezaji wa sabuni na ushonaji, ununuzi wa vyerehani 42 kwa ajili ya vikundi vya ushoni.

Pia, ameeleza kuwa Mradi wa EBARR unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa upande wa wilaya ya Kaskazini ’A’ umefanikisha ununuzi wa mizinga ya nyuki 200 na ujenzi wa nyumba za nyuki (manzuki), mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vyote, kuanzishwa kwa vitalu vya miche ya miti 56,000 na utengenezaji wa majiko banifu kwa kaya 125.

Aidha, Naibu Waziri Khamis amesema mradi huo na miradi mingine inafanyiwa ufuatilaji ili kuona kama inatekelezwa kwa ufanisi na wananchi wananufaika nayo.

Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais inawatumia maafisa viungo waliopo katika halmashauri na maafisa mazingira wa wilaya na mikoa katika ufuatialji.

Halikadhalika, amesema kupitia ziara za viongozi hususan Kamati za Kudumu za Bunge zinazosimamia Mazingira na viongozi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ufuatiliaji wa ufanisi wa miradi unafanyika.