Mradi JNHPP wapunguza athari za mafuriko Rufiji

RUFIJI, Pwani: MKUU wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle amesema kuwa mradi wa kufua umeme wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) umepunguza kwa kiasi kikubwa mafuriko na athari zake yaliyokuwa yakitokea wilayani humo.

Meja Gowelle ameyasema hayo katika mazungumzo yake na wawakilishi kutoka Shirika la Umeme, TANESCO, walipotembelea wilayani kwake baada ya kukagua, kujionea na kufanya tathmini ya athari mbalimbali zilizojitokeza kutokana na mafuriko yaliyotokea.

Amesema kuwa kujengwa kwa JNHPP lilikuwa wazo zuri na kumerahishisha kitaalamu kujua kiwango cha maji kinachotolewa kwenda kwa wananchi na hivyo kufanya athari kuwa ndogo ikilinganishwa na namna ilivyokua wakati bwawa halijajengwa ambapo mafuriko yalikua yanatokea bila kujua kiwango cha mtiririko wa maji.

“Miaka hiyo ya nyuma kulikuwa hakuna tahadhari. Wananchi walikuwa wakijishtukia tu maji yamejaa katika nyumba zao na mashamba yao. Kipindi hiki sisi kama serikali tuliweza kupata tahadhari ya mapema kutoka TANESCO hivyo tuliweza kufikisha taarifa kwa wananchi na kuwezesha kujinusuru. Na ndio maana mpaka sasa hakuna kifo hata kimoja kilichoripotiwa kutokea kutokana na maji,” amesema Meja Gowelle.

Ameeleza kwa kiasi kikubwa tahadhari na taarifa zilitolewa mapema kwa wananchi na hvyo kusaidia kupunguza athari kwenye maisha ya watu ukilinganisha na mashamba ya mazao mbalimbali kama mahindi,mpunga nk kuharibika.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Abdul Bakari Chobo amesema mafuriko Rufiji ni suala la miaka mingi tangu yeye anazaliwa anakua akiyaona lakini ni ukweli dhahiri kwamba Bwawa la Julius Nyerere limepunguza makali ya mafuriko kwani hawakuwahi kupata mafuriko kabisa miaka ya hivi karibuni.

”kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha kwenye ukanda wa nyanda za juu kusini maji yamekua mengi na hivyo iwapo Bwawa lisingekuwepo huenda madhara yangekua makubwa zaidi nawasihi watu kuacha upotoshaji wa taarifa kuwa sababu kubwa ya mafuriko ni ujenzi wa bwawa tunatumaini litakapokamilika litapunguza zaidi athari hizi na kwa sisi kama Rufiji mradi umetusaidia mambo mengi sana sana tunapata service levy tumejenga mashule nakadhalika,” amehitimisha.

Habari Zifananazo

Back to top button