Mradi wa maji kunufaisha wananchi wa Mutukula

MISSENYI, Kagera: Wananchi wapatao 7,562 kutoka vitongoji vinane katika kijiji cha Mutukula wilayani Missenyi mkoani Kagera wanatarajiwa kunufaika na mradi wa maji wa kijiji hicho ambao umefikia asilimia 70.
Mradi huo uliogharimu Sh bilioni 1.4 utaongeza upatikanaji maji kutoka asilimia 86 ya sasa hadi 100.
Kiongzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi ametembelea mradi huo na kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji ambapo amesema hayo ni maono ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi hawatembei mwendo mrefu kufuata huduma ya maji.

“Tumeridhishwa na utekelezaji wa mradi huu ambao unahudumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) tunawaomba wanachi wa vitongoji vitano ambavyo bado havijapata maji tuwe wavumilivu mradi unakamilika muda si mrefu tunapata maji safi na salama,”amesema Ussi.
Mratibu wa mradi, Mhandisi Lucas Selebeya, Meneja Buwasa Wilaya ya Missenyi alisema mradi huo ujenzi ulianza Januari 2025 umefikia asilimia 70 ambapo vitongoji vitatu kati ya vinane vinapata huduma ya majisafi na salama unatarajiwa kukamilila Desemba 30 mwaka huu.

Thadeo Kashalala ni mmoja wa wananchi ambao wameunganishiwa huduma ya maji ambapo amesema wanashukuru serikali kwa kuleta mradi huo, kwani walikuwa wakitumia maji machafu kutoka kwenye madimbwi ambayo wananyweshwa mifugo huku wakati wa kiangazi walitembea kilometa 10 kufuata maji mto Kagera.



