Mradi wa Parachichi waongeza ajira kwa vijana Ngara

NGARA, Kagera: Kikundi cha vijana wanane wa Kata ya Kabanga wilayani Ngara mkoani Kagera ambao wamejiunga na kuanzisha kilimo cha matunda aina ya parachichi wamekuwa kichocheo cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi kupitia kilimo zao hilo.
Utekelezaji wa Sera ya Vijana ya mwaka 2017 hadi 2034 imeisukuma Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kutenga Sh milioni 52.6 kati ya hizo Sh milioni 40 ni asilimia 10 itokanayo na mapato ya ndani huku vijana wakichangishana fedha taslimu kupitia kikundi chao hadi kufikia Sh milioni 200.
Mwenyekiti wa kikundi cha Kabanga matunda group,Livingstone Shedrack ametoa taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi na kusema kuwa lengo la vijana hao kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ngara ni kuhakikisha vijana wanajipatia ajira na kipato pia mradi huo hutumika kujinfunza kilimo cha parachichi kutafuta masoko ili kuuza na kupata faida.
Amesema mradi huo wenye ekari 24.05 umegharimu zaidi ya Sh milioni 252.6 ambapo Sh mililioni 200 zinatokana na maamuzi ya wanakikundi wanane kuamua kuanzisha mfuko wa kuweka na kukopa ili waanzishe mradi utakao wainua na kuondokana na umaskini .
“Manufaa ya mradi huu vijana 200 kutoka ndani ya Kata ya Kabanga wamepata ajira ambapo inawasaidia kujiongezea kipato,kusaidia watu wenye mahitaji maalum ikiwemo watoto na wazee,tumekuza biashara zetu kwa kuanzisha vituo vitano vya ukusanyaji wa parachichi kutoka sehemu mbalimbali na kuwauzia wafanyabiasha wakubwa,”ameeleza Shedrack .
Msafiri Joseph na Nickson Nicodemas ni wanakikundi wanasema matamanio yao ni kuona kila kijana aliyeko nje ya kikundi anajiunga na anapata fursa hiyo ya kujiajiri kwasababu wao walianza wakifanya kazi za vibarua kwa matajiri kwa kukusanya parachichi hari iliyowafungua kiakili na kujiajiri.
kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ussi wakati akizindua mradi huo amepongeza ubunifu wa vijana hao na kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono ili wafikie malengo yao kwasasa na kudai kuwa hayo ni matamanio makubwa ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuona vijana wanajiingizia kipato kwa njia halali.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara kanali Mathias Kahabi amesema Mwenge umezindua miradi saba yenye thamani ya Sh bilioni 2.7.



